Bei mafuta ya petroli, dizeli zashuka

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imetangaza bei kikomo ya mafuta ya petroli kupitia Bandari ya Dar es Salaam inayoanza kutumika leo tarehe 5 Juni 2024, kuwa imeshuka kwa Sh52.72 na kufikia Sh3, 261 kwa lita moja, ikilinganishwa na bei ya mwezi uliopita. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Taarifa iliyotolewa Ewura leo Jumatano imeonyesha bei ya dizeli inayochukuliwa kwenye bandari hiyo ya Dar es Salaam pia imeshuka hadi Sh3,112 kutoka Sh3,196 iliyokuwa inatumika mwezi uliopita.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa kupungua huko kumetokana na kupungua kwa bei ya mafuta yaliyosafishwa katika soko la dunia (FBO) kwa wastani wa asilimia 11.82 kwa petroli na asilimia 7.77 kwa dizeli na asilimia 7.94 kwa mafuta ya taa.

“Pia kuongezeka kwa wastani wa gharama za kubadilisha fedha za kigeni (Applicable Exchange Rate) kwa 1.4%; kupungua kwa gharama za uagizaji wa mafuta (premiums) kwa wastani wa asilimia 2.06 kwa petroli na asilimia 8.51 kwa dizeli katika Bandari ya Dar es Salaam;

“Kuongezeka kwa gharama za uagizaji wa mafuta kwa wastani wa asilimia 7.07 kwa petroli na asilimia 25.24 kwa dizeli katika Bandari ya Tanga; na kupungua kwa wastani wa asilimia 12.64 kwa mafuta ya petroli na 12.61 kwa mafuta ya dizeli katika Bandari ya Mtwara,” imesema taarifa hiyo iliyosainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Dk James Mwainyekule.

Dk James Mwainyekule.

Aidha, kwa Bandari ya Tanga bei ya petroli imeshuka hadi Sh3,263 kutoka Sh 3,360 kwa mwezi uliopita kwa upande wa dizeli nayo imeshuka hadi Sh 3,121 kutoka Sh 3,242.

Katika Bandari ya Mtwara petroli imeshuka na itauzwa kwa rejareja kwa Sh 3,267 kutoka Sh 3,317 kwa mwezi uliopita na dizeli itauzwa Sh3,122 kutoka Sh3,200 mwezi uliopita.

Related Posts