CTI yataka sheria nzuri kuwalinda wenye viwanda

Dar es Salaam. Kuwa na sheria nzuri ya kuwalinda wafanyabishara wa viwanda, kumetajwa kuwa ni moja ya vichocheo vya kuongeza kasi ya uwekezaji katika sekta hiyo.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano Juni 5, 2024 na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirikisho la Wenye Viwanda nchini (CTI) Leodegar Tenga, wakati wa hafla ya kuingia mkataba wa ushirikiano kati ya CTI na Tume ya Ushindani nchini (FCC).

Mkataba huo, unalenga namna bora ya kubadilishana taarifa kwenye utekelezaji wa sheria ya utambuzi wa bidhaa zinazozalishwa.

“Sekta ya viwanda bado haifanyi vizuri katika kuchangia uchumi wa Taifa. Sitaki kwenda kwenye takwimu zaidi lakini wenzetu wanafanya vizuri kwa kuwa wanazingatia zaidi sheria, kuhakikisha mazingira yanakuwa rafiki,” amesema.

Amesema wawekezaji wanapokuja nchini, kuna mambo huwa wanategemea hususan katika sekta ya viwanda na inakuwa tofauti na yule anayekuja kufanya biashara za kawaida.

Tenga amesema wafanyabiashara ni tofauti na wenye viwanda, kwani wao huangalia mazingira nini kinahitajika kisha huagiza bidhaa na kuja kuuza, lakini wenye viwanda lazima watafute ardhi, wajenge, walete vifaa na waajiri kwahiyo uwekezaji ni mkubwa kabla hawajaanza kuzalisha.

Amesema wawekezaji wa viwanda ni watu wanaohitaji unyeti wa mazingira mazuri ya kufanya shughuli zao, kiasi cha kuweza kurejesha mitaji yao waliyotumia kuwekeza.

“Sasa wakija hapa kuangalia asilimia 80 ya soko ni bidhaa bandia anasononeka kwa hiyo FCC, wana wajibu wa kutengeneza mazingira mazuri ya biashara kwa wenye viwanda,” amesema

Amesema uendeshaji wa viwanda ni mgumu, unahitaji muda na uvumilivu kiasi kwamba inachukua hadi miaka mitano kuanza kurudisha kile mwekezaji alichowekeza.

Akizungumzia makubaliano hayo, Mkurugenzi Mkuu wa (FCC) William Erio amesema wameingia mkataba huo kwa kuwa jukumu lao ni kulinda na kukuza ushindani ili kulinda ukuaji na maendeleo ya sekta ya viwanda nchini.

“Tunataka ushindani wa bidhaa nchini uwe sawa pande zote, pamoja na kulinda lakini katika ushirikiano wetu kwa pamoja tutahakikisha tunazuia vitendo vinavyoweza kuathiri ushindani na kuvuruga uwekezaji wa sekta ya viwanda kwa ujumla,” amesema Erio.

Erio amesema kupitia mkataba huo ni pamoja na watu wenye viwanda kuingia makubaliano pasina kuzingatia sheria za ushindani, huku akieleza makubaliano hayo wanaamini viwanda vitatekeleza majukumu yake kwa uhuru na hawataingia kwenye zabuni kwa mbinu hadaifu.

“Tutazingatia sheria ya alama ya bidhaa kuhakikisha hakuna bidhaa bandia zinaweza kuingia au kupita na kuzalishwa nchini. Tumeona tukifanya kazi pamoja ya kupeana elimu na kuelekezana na CTI kupitia muungano wao,  tutawafikia wahusika na kuzuia uzalishaji wa bidhaa bandia,” amesema Erio.

Related Posts