Mwanamke asimulia alivyochomwa moto, kushambuliwa kwa panga sehemu za siri

Mtwara.  Hakika sio rahisi kusikiliza simulizi ya Elizabeth Hashim (38),  mkazi wa kijiji cha Makong’onda Wilayani Masasi mkoani Mtwara.

Moja ya matukio makubwa ya ukatili aliyopitia kwenye ndoa yake ni kuchomwa moto sehemu zake za siri na baada ya kujiuguza na kupona, akaingizwa panga.

Ilifika hatua mwanamke huyo aliona kuwa kipigo, manyanyaso na mateso kwenye ndoa yake ni jambo la kawaida mpaka siku majirani walipoamua kuingilia kati ili kumuokoa.

Mateso ya Elizabeth kwenye ndoa yake, ndiyo yaliyolifanya Mwananchi kupiga kambi nyumbani kwake, katika kijiji cha Makong’onda ili kupata simulizi halisi.

Mei 7, 2024 Mahakama ya Wilaya ya Masasi ilimhukumu mumewe, Abdallah Mataka (56) mkazi wa kijiji cha Makong’onda kwenda jela miaka mitano baada ya kumkuta na hatia.

Kesi namba 203 iliendeshwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Masasi. Batista Kashusha. Hii ikawa mwanzo wa maisha mapya ya Elizabeth.

Simulizi yake Elizabeth unaweza kuioanisha na utafiti uliofanywa na mtandao wa TDHS walioufanya 2015/2016 ambao unaonyesha katika kila wanawake kumi, watatu kati yao wamewahi kufanyiwa vitendo vya ukatili.

Utafiti huo pia unaonesha wanawake  wanne kati ya 10, wamewahi kukumbana na ukatili wa kimwili tangu wakiwa na umri wa miaka 15.

Aidha, takwimu hizo zinaonesha asilimia 58 ya wanawake na asilimia 40 ya wanaume wanakubali kwamba ni sahihi mume kumpiga mke wake kwa sababu mbalimbali.

Hivyo, hata Elizabeth anaweza akawa miongoni mwa wanawake hao ambao wamepitia mateso ndani ya ndoa zao.

Akizungumza na Mwananchi, Elizabeth anasema siku alipoingizwa panga sehemu zake za siri na mumewe Mataka, wasingekuwa majirani zake kumsaidia, huenda angepoteza maisha.

Anasema siku hiyo alitoka nyumbani huku mume wake akimfuatilia kila alipokuwa anaenda kwenye shughuli zake.

Muda wa kurejea nyumbani ulipofika, akaraudi  nyumbani alipokuwa eneo la nyumbani kuna kitu alikiangusha ambacho hata hivyo hakikumbuki akainama kukiokota, lakini ghafla akashambuliwa kwa kipigo kutokea nyuma yake na akajikuta akianguka chini akiwa ametanguliza tumbo na alikuwa mjamzito.

Anasema alipokuja kugeuka akamuona mumewe ndiye aliyemshushia pigo lile lililomdondosha chini huku akijua ni mjamzito.

“Sikujua kwa nini ananipiga, ila siku ile alikuwa kama mlinzi wangu, ilikuwa kila ninapoenda alikuwa akinifuata, na pale nyumbani alinipiga sana mpaka nikapoteza fahamu kwa sababu alinibamiza pia ukutani,” anasimulia mama huyo.

Alipoulizwa sababu ya kupigwa, anasema hakutaka niwapatie chakula wanangu, ambao nilizaa na mwanaume mwingine, kabla hatujaoana.

Hata hivyo, anasema mateso na vipigo kutoka kwa mumewe huyo ni vya muda mrefu na wameshasuluhishwa sana, lakini mume hakubadilika hadi siku alipotekeleza tukio hilo lililompeleka jela.

Amesema mbali ya kipigo hicho siku hiyo, Mataka aliona haitoshi, alichukua panga akamuingiza sehemu za siri huku wanawe wawili walikuwa wakishuhudia ndipo wakaamua kuomba msaada kwa majirani.

Wifi yake Elizabeth, aliyejitambulisha kwa jina la Zainabu Hassan ambaye anaishi nao jirani anasema alisikia kelele za mtu akipiga yote.

Alipogundua ni sauti ya wifi yake, alikimbilia nyumbani kwao na kukuta mume akiendelea kumpiga mkewe licha ya damu nyingi kumwagika sehemu za siri.

“Yaani nilisikia yowe mwanamke analia kwa uchungu nikaamka nikakimbilia eneo la tukio  nilipofika nilikuta mke yuko chini mume yuko juu nikaamua kusimama kati yao ili mwanaume aache kumpiga mkewe,” anasema Zainab

Amesema kitendo cha kuamulia ugomvi huo kilimuudhi kaka yake ambaye alitaka kuanza kumpiga na yeye.

“Nikamuuliza mumewe kulikoni, hakujibu kitu akatoka nje, nikataka kumnyanyua mkewe nikashtuka kuona damu nyingi zikichuruzika niliogopa,” amesema Zainab.

Amesema alipoona damu kwa mara ya kwanza alihisi wifi yake yuko kwenye siku zake, lakini alipomfunua nguo na kuona zinavyomwagika kwa wingi, ilibidi aombe msaada kwa majirani.

 “Wifi yangu alipoteza fahamu, nilipoangalia pembeni niliona panga limetapakaa damu, niliita majirani tumwahishe hospitali ili kunusuru maisha yake,” anasimulia dada huyo.

Naye Baraka Salum anasema alishuhudia mateso ya jirani yake baada ya kuitwa siku ya tukio.

 “Nilipigiwa simu kutoka kwa mwenyekiti na mgambo juu ya tukio ambalo lilimkuta mtoto wa mjomba wangu (Elizabeth) kuwa amechomwa na kitu chenye ncha kali, niliwahi kwenda lakini alikuwa tayari yuko kituo cha afya Makong’onda, lakini baadaye madaktari waliamua kumhamishia Hospitali ya Newala kwa matibabu zaidi,” anasimulia Salum.

Mwenyekiti asimulia alivyosuluhisha

Mwenyekiti wa Kijiji cha Makong’onda, Hamis Millanzi anasema kwa muda mrefu amekuwa msuluhishi wa ndoa ya Elizabeth na Mataka.

Amesema haikuwa ikipita siku mbili bila kutokea tukio lolote yakiwemo ya ukatili kwenye familia hiyo.

 “Hata siku ya tukio, saa moja jioni  nilipata simu ya mtu kuchomwa na upanga  sehemu za siri,  nilikimbilia eneo la tukio ambapo kweli nilikuta yule mwanamke akiwa amelala chini huku damu zikimmwagika, tukamchukua na kumpeleka hospitali,” amesema Millanzi.

Hata hivyo, anasema wanamshukuru Mungu mama huyo hakupoteza ujauzito wake aliokuwa nao.

Lakini ujauzito ule ulipofikisha miezi minane, alijifungua na mtoto alifariki dunia.

Baadhi ya majirani waliozungumza na Mwananchi wanadai Elizabeth aliposhikwa na uchungu, alichelewa kwenda hospitali na akajikuta akijifungulia nyumbani mtoto huyo ambaye aliyefariki dunia.

Siku alipochoma nyumba moto

Elizabeth anasema kuna siku alimtaka yeye na watoto watoke nje ya nyumba akidai anataka kufanya dawa, lakini alimgomea.

“Ilipofika usiku alitoka nje akachukua kijinga cha moto na kurusha juu ya paa la nyumba yetu ambayo tuliiezeka kwa nyasi, inaonyesha wazi alikuwa amedhamiria kutuua na wanangu,” amesema Elizabeth.

Amesema bahati nzuri usiku ule, binti yake alikuwa hajalala, alikuwa akisoma ndiye aliyebaini kwamba nyumba inawaka moto.

“Ule usiku ni kweli alidhamiria kuua kabisa ila binti yangu mkubwa alikuwa macho akisoma, aliona moto akakimbia kujiokoa halafu akaniamsha nikamuokoa mtoto wangu wa  kiume ambaye nilimrusha nje kupitia dirishani,” amesema Elizabeth.

Hata hivyo, mwanamke huyo amesema pamoja na mateso yote hayo, bado anampenda mumewe anaamini ipo siku atabadilika.

Anasema siku alipochomwa moto sehemu za siri, uongozi wa kijiji waliamuru mume amuuguze mke huyo mpaka apone lakini hakwenda hospitali.

“Lakini nilimpenda ndio maana niliolewa naye kwa kuwa nilimtaka mwenyewe licha ya kujua changamoto zake, lakini pia nilichoka kukaa mwenyewe nikaridhia kuolewa naye,” amesema.

Elizabeth amesema mume wake alikuwa na wivu kiasi cha kufanya matukio mengi ya kumuumiza bila huruma.

“Alikuwa akinipiga hata mbele ya watoto, alikuwa hanionei huruma hata kidogo,” amesema Elizabeth.

Anasema siku ya tukio alipigwa kiasi cha majirani kuingilia kati wakimchukua na kumkimbiza katika kituo cha afya na baadae Hospitali ya Wilaya ya Newala ili kuokoa uhai wake.

Simulizi ya kuchomwa moto sehemu za siri

Elizabeth anasema kipigo na mateso ilikuwa sehemu ya maisha yake.

Amesema kilichofanya aendelee kuvumilia mateso hayo ni baada ya kukata tamaa ya kuishi.

Anasimulia kuwa mume wake aliwahi kuchukua majani makavu akayaweka sehemu zake za siri kisha kuwasha moto na hakuchukuliwa hatua zozote.

“Siku aliyonichoma moto sehemu za siri alinipiga akanifunua nguo akaweka nyasi na kunichoma moto akidai kuwa mimi malaya nina wanaume wengi niliumia sana, lakini nilikaa nyumbani najiuguza mpaka nikapona,” anasema Elizabeth.

Anasema mumewe huyo alikuwa akimtuhumu kwamba sio mwamifu, japo hajawahi kumuona kwenye uhusiano na mwanaume mwingine.

 “Hadi chooni alikuwa akinisindikiza, kwa sababu ya wivu. Tulikuwa tukipita mashambani kuomba vibarua kisha tunafanyakazi na kupata hela zilizokuwa zinatusaidia kuendesha maisha, hata hivyo kuchungana chungana kulifanya tukose kazi nyingi,” amesema.

Elizabeth ni mke mdogo, taarifa zinaonyesha kuwa mke mkubwa ambaye alifariki pia aliwahi kupitia ukatili kutoka kwa Mataka.

Pamoja na kuwa Elizabeth alimfahamu mume huyo, lakini alikubali akiamini, kwake haitakuwa kama kwa mwenzake.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa wa Mtwara Kitengo cha Ustawi wa Jamii kupitia maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili yaliyofanyika mwaka 2023 wilayani Masasi, takwimu zilionyesha kipindi cha Januari hadi Septemba 2023 zaidi ya matukio ya ukatili 1,120  yalilipotiwa.

 Katika matukio hayo, watoto walikuwa 684 na watu wazima 436 na zaidi ya mashauri 128 yalifikishwa mahakamani na makosa  20 yalihukumiwa huku makosa 892 yakiishia katika ofisi za ustawi wa jamii.

 Aidha, makosa 20 yanaendelea huku makosa 40 yakiwa bado yako kwenye uchunguzi na makosa 20 yalichepushwa ambapo kwa watu wazima makosa ya ukatili wa kimwili yalikuwa 149 na ya kingono yalikuwa 31.

Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Pindi Chana wakati akifungua maadhimidho ya siku 16 za kupinga ukatili Desemba, 2023 jijini Dodoma,  alisema takwimu zinaonesha kuwepo kwa ongezeko la matukio ya ukatili wa vipigo na kujeruhiwa kwa wanawake.

Alisema tayari Serikali imeanza mkakati wa kukabiliana navyo,  huku akiitaka jamii kutoa taarifa kwa vyombo vya sheria ili wahusika wachukuliwe hatua.

Makala hii imeandikwa kwa ufadhili wa Bill & Melinda Gates Foundation

Related Posts