Benki ya Korea yaipa Serikali mkopo Sh427 bilioni ujenzi wa hospitali Zanzibar

Seoul. Serikali ya Tanzania imepokea mkopo wa Dola za Marekani 163.6 milioni (Sh427.8 bilioni) kutoka Benki ya Exim ya Korea, kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Binguni Zanzibar pamoja na kituo cha mafunzo ya utabibu.

Mkataba wa mkopo huo umesainiwa leo Jumatano Juni 5, 2024 kati ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk Natu Mwamba na Mkurugenzi Mtendaji Mwandamizi wa Benki ya Exim ya Korea, Hwang Kiyeon na kushuhudiwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais wa Zanzibar, Fedha Dk Saada Mkuya.

Mkataba huo wa mkopo umetiwa saini wakati Rais Samia Suluhu Hassan akiendelea na ziara yake ya siku sita nchini Korea.

Akizungumzia mkopo huo, Waziri Mkuya amesema kwa muda mrefu wananchi wamekuwa wakisubiri kuanza kwa mradi huo na sasa baada ya kusainiwa kwake, watakata kiu yao kwa mradi huo kuanza kujengwa.

Amesema mradi huo utasaidia kuboresha huduma za afya kwa wananchi, pamoja na kuwajengea uwezo madaktari watakaopata mafunzo kwenye kituo kitakachojengwa visiwani humo hasa kwenye eneo la teknolojia ya vifaa tiba.

“Mradi huu ni wa miaka mitano lakini kwa sababu ya umuhimu wake kwa wananchi, tutajitahidi uende haraka ili wananchi waanze kupata huduma mara moja,” amesema Dk Mkuya.

Ameongeza kuwa hospitali hiyo itajikita katika utoaji wa huduma kwenye maradhi ya watoto, wazazi na matibabu ya moyo. Amesema itakuwa na vifaa vya kisasa vya matibabu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Exim ya Korea, Kiyeon amesema mkopo huo umetokana na ushirikiano mzuri kati ya serikali za Tanzania na Korea Kusini, huku akitarajia ushirikiano huo utaendelea kwenye maeneo mengine.

“Hospitali hii itawekewa vifaa vya teknolojia ya juu, itakuwa na vitanda 600. Tunatarajia kwamba itaboresha utoaji wa huduma za afya huko Zanzibar,” amesema Kiyeon na kusisitiza kwamba wataendelea kuimarisha ushirikiano na Serikali.

Related Posts