Chama cha Wanasheria cha Tanganyika (TLS), kimewataka wandishi wa habari nchini kuzitumia sheria zilizopo kuhakikisha wanausaidia umma katika ukuzaji wa uhuru wa kujieleza. Anaripoti Wellu Mtaki, Dodoma… (endelea).
Hayo yameelezwa jana tarehe 4 Juni 2024 jijini Dodoma na Makamu Mwenyekiti wa TLS Wakili Deus Nyabiri alipofungua mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari juu ya uhuru wa kujieleza.
Amesema nchini kuna vyombo vingi vinavyotoa habari hivyo ni wajibu wa TLS kuwajengea uwezo watoa habari wa vyombo hivyo ili kutambua wajibu huo ipasavyo na kuelimisha umma umuhimu wa kutumia uhuru huo wa kujieleza.
“Katika katiba kuna suala la haki za binadamu, mojawapo ni haki ya kujieleza, haki ya kupata habari, haki ya kutoa taarifa. Yote ni mambo muhimu kwa binadamu. Tunavyo vyombo vya habari mbalimbali vinavyotoa taarifa kwa jamii kuhusu mambo mbalimbali hivyo ni wajibu wa TLS kuwajengea uwezo wanaotoa taarifa ya maendeleo ya nchi,” amesema Nyabiri.
Nyabiri amesema anaamini katika mafunzo hayo kila mwana taaluma atatoka na mtazamo chanya ambao utamsaidia katika kuchanganua habari zinazofaa na zisizofaa katika jamii.
“Imani yangu ni kuwa kila aliyepo hapa atatoka na elimu ya kutosha lakini namna ya kuitumia elimu hiyo ndio changamoto kwa sababu anaweza kupata elimu lakini akaingiwa na mihemko ya kibinadamu akaleta kitu tofauti hivyo hapa tunaamini watapata kitu chanya cha kusaidia kujua kuwa habari hii inafaa katika jamii au habari hii jamii haiwafai,” amesema Nyabiri.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Tathimini na ufatiliaji TLS, Seleman Pingoni amesema semina za aina hiyo hutolewa kwa sababu kulikuwa na malalamiko ya kutoridhishwa katika suala la utoaji wa haki.
“TLS imeamua kutoa mafunzo haya kwa sababu Taifa lilipitia sheria mbalimbali zilizotungwa na kulikuwa na malalamiko ya wanahabari na wana-azaki wakielezea kuhusu kutoridhishwa kwao na namna ambavyo haki yao ya kutoa mawazo inavyominywa na sheria,” amesema Pingoni.
Kwa upande wake Afisa Ulizi kwa Umma wa TLS, Jacqueline Mwingwa amesema uhuru wa kujieleza ni nyenzo muhimu katika masuala ya kidemokrasia hivyo kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaani, udiwani, ubunge na urais vyombo vya habari vitapata uwezo wa kufanya kazi kuna huru na haki.
“Semina hii inaenda kuwajengea kujiamini kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa, udiwani, ubunge na urais kama tunavyoelewa uhuru wa kujieleza ni moja kati ya nyenzo muhimu katika masuala ya kidemokrasia na watapata uwezo kwa kufanya uchaguzi kwa haki na huru” amesema Mwingwa.
Chama Cha Tanganyika Low Society kiliazishwa kwa Sheria na ndani ya Sheria hizo Kuna mambo ambayo chama kinapaswa kusaidia jamii, Bunge, Mahakama na vyombo vyote.