Dar es Salaam. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amezitaka jumuiya za kimataifana na nchi za Afrika, kubeba changamoto za wavuvi wadogo wanaobeba sekta ya uvuvi Afrika.
Biteko ameyasema hayo leo Juni 5, 2024 jijini hapa alipokuwa akifungua mkutano wa uvuvi kwa washiriki zaidi ya 470 kutoka mataifa 32 ya Afrika.
Mkutano huo pia unajumuisha maadhimisho ya miaka 10 ya utekelezaji wa Mwongozo wa Uvuvi Mdogo na Muundo wa kisera wa kusimamia Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji barani Afrika.Pia utaangazia fursa zilizopo katika uchumi wa buluu.
Amewataka wajumbe wa mkutano huo kujadili changamoto za wavuvi wadogo kwa ajili ya kuzipeleka katika mkutano wa kimataifa utakaofanyika Roma Italia Julai mwaka huu.
“Lengo ni kutoa wito wa pamoja kwa jumuiya za kimataifa na zenyewe kwa pamoja kuweka sauti ya pamoja ya kuwapigania na kuwasemea wavuvi wadogo, ambao ndio wenye mchango mkubwa kwenye sekta ya uvuvi,” amesema.
Huku akirejea msemo wa Kiingereza unaosema, Look after the pennies the pounds will look after themselves (zilinde fedha ndogo, fedha kubwa zitajilinda zenyewe) alisema kuja haja ya kuwajengea uwezo wavuvi wadogo.
“Kwa maana hiyo, mkiwashirikisha wavuvi wadogo, mkawafundisha mbinu za kisayansi za kuvua bila kuharibu mazingira, bila shaka wavuvi wakubwa watakuja wenyewe kadiri mnavyoendelea,” amesema.
Akitaja takwimu, Biteko amesema Tanzania inazalisha tani 472, 579 za samaki kwa mwaka na kati ya hizo, tani 429,168 zinatokana na uvuvi katika maji ya asili.
“Kiasi cha fedha kinachotokana na uvuvi kwa mwaka ni Sh3.4 trilioni na sekta inakua kwa asilimia 1.9 kwa mwaka na inakadiriwa kutoa ajira za moja kwa moja watu 230,000, huku ajira zinazoendana na uvuvi kwa Tanzania waoatao milioni sita. Wadogo wanachangia asilimia 95 ya uvuvi wote, hivyo pasipo wao, hakuna uvuvi nchini,” amesema.
Amesema Serikali itaendelea kuanzisha viwanda kwa ajili ya uchakataji wa samaki, mahali pa kuhifadhia au kugawa boti za uvuvi za kisasa, vizimba vya kufugia samaki na zana zinazohusika na kutoa pembejeo za kufugia samaki kama chakula na vifaranga na kutoa misamaha ya kodi kwa uagizaji wa bidhaa za samaki.
Amezitaja changamoto za wavuvi kuwa pamoja na athari za mabadiliko ya tabia nchi, akisema hilo ni suala la Afrika kwa ujumla, hivyo ni lazima kuwa na juhudi za pamoja.
“Changamoto nyingine ni ushirikishwaji mdogo wa wadau katika usimamizi wa shughuli za uvuvi hususani wanawake na vijana na upotevu wa mazao ya uvuvi,” amesema.
Awali akimkaribisha Dk Biteko, Waziri wa Uvuvi na Mifugo, Abdallah Ulega amesema mkutano huo ni mwendelezo wa mkutano wa wavuvi wadogo uliofanyika Roma Italia Machi 2023, ambapo yeye alieleza utayari wa Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano wa Afrika.
“Mkutano huu utatumika kama jukwaa litakalokutanisha wavuvi wetu na wenzao kujadili mafanikio na changamoto zinazowakabili dhidi ya mustakabali wao,” amesema.
Akitoa salamu katika mkutano huo, Rais wa wataalamu wa uvuvi wa Afrika, Gaoussou Gueye amesema kuwa mkutano huo utajadili kwa kina fursa za uvuvi na changamoto za ajira na jinsi ya kuzitatua.
“Kimsingi, uvuvi mdogo ndio unatakiwa kuwa moyo wa uchumi wa buluu, hivyo ni muhimu kuwalinda wavuvi wadogo,” alisema.
Naye Mkurugenzi mkazi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Dk Tipo Nyabenyi, amesema wanawake ni kundi linalotoa mchango mkubwa katika uvuvi mdogo akitaka wawezeshwe zaidi.
“Wanawake watatu kati ya watu 10 wanashiriki katika uvuvi wakichangia katika uchumi na lishe,” amesema.
Naibu Katibu mkuu wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (Sadc), Angele Makombo N’Tumba naye amesema mkutano huo umekuja wakati jumuiya hiyo ikiwa imepitisha mkakati wa uchumi wa buluu na itifaki ya uvuvi.