YANGA mwendo wa fedha tu. Baada ya kujihakikishia kuvuna Sh 600 Milioni kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kutoka kwa wadhamini wa ligi hiyo, wababe hao wa soka nchini jana wamevuna fedha nyingine zaidi ya nusu bilioni kutoka kwa Mdhamini Mkuu wa klabu hiyo, Kampuni ya SportPesa.
SportPesa jana iliikabidhi klabu hiyo mfano wa hundi ya Sh 537.5 Milioni ikiwa ni bonasi ya kutwaa ubingwa Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho na kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2023-2024.
Hafla ya makabidhiano ya hundi hiyo yalifanyika jana jijini Dar es Salaam, ikuhusisha Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa SportPesa, Tarimba Abbas na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa kampuni hiyo, Sabrina Msuya, huku kwa Yanga kulikuwa na Ofisa Mtendaji Mkuu, Andre Mtine na Rais Injinia Hersi Said pamoja na benchi la ufundi na baadhi ya wachezaji walishiriki hafla hilo.
Awali Sabrina aliipongeza Yanga kwa mafanikio iliyoyapata msimu huu ikiwamo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho na kuitinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa ni baada ya kupita miaka 25 iliposhiriki michuano hiyo hatua ya makundi mwaka 1998.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Tarimba alianza kwa kuwapongeza wachezaji, benchi la ufundi na viongozi wa Yanga kwa kulitwaa kombe hilo mara tatu mfululizo na kuongeza;
“SportPesa siku zote imekuwa ikijivunia mahusiano ya kiudhamini kati ya kampuni na Yanga na haijawahi kutokea tukajutia kwa sababu tumejihusisha na klabu inayoendeshwa kiuweledi.”
Tarimba aliupongeza uongozi wa klabu hiyo kwa kujenga timu imara yenye benchi la ufundi bora kiasi kwamba Yanga imekuwa ni timu inayojitosheleza kwa ushindani wa aina barani Afrika. “Ni jambo ambalo SportPesa tunaona tumefikia malengo yetu.
Kila tunachokiahidi kimkataba tumekitekeleza bila kuchelewa na Yanga inahitaji mdhamini wa sampuli kama SportPesa. Leo tumekabidhi mfano wa hundi ya shilingi 537.5M.”Alisema Tarimba na kuongeza;
“Tunaomba Yanga wasibweteke, waendelee kuboresha timu yao, kwani tunaona mwaka 2024/25 utakuwa ni mwaka wa ushindani sana.” Kwa upande wa Yanga, Rais Hersi Said alishukuru kwa ushirikiano wanaoupata kwa mdhamini mkuu katika kutekeleza mipango na majukumu ya kila siku.
“Nichukue nafasi hii kuishukuru SportPesa kwa kutekeleza kwa wakati makubaliano yaliyopo kwenye mkataba kwa kutoa bonasi ya Sh 537,500,000 baada ya klabu kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho na kufika robo ya Ligi ya Mabingwa ya CAF. Huu ni msimu wa tatu mfululizo tumekuwa tukichukua ubingwa na kupata bonasi hizi kutoka SportPesa.
“Tunawaahidi SportPesa, tutaendela kujenga timu imara ya ushindani ndani na nje ya Tanzania ili kuitangaza zaidi SportPesa ambaye ndiye mdhamini wetu mkuu.” Huu ni mwaka wa sana tangu SportPesa kuanzishwa kwake huku ikiadhimisha miaka saba tangu kuanza shughuli ya kudhamini klabu ya Yanga.