Dar es Salaam. Mwenyekiti wa zamani wa Chadema Kanda ya Nyasa, Peter Msigwa amefika mkoani Singida kuungana na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu kwenye mikutano ya hadhara.
Lissu amekuwa na mikutano ya hadhara mkoani Singida tangu mwanzoni mwa Juni inayotarajiwa kufanyika kwa wiki tatu.
Msigwa aliyeshindwa na Joseph Mbilinyi (Sugu) katika uchaguzi wa Kanda ya Nyasa uliofanyika Mei 30, 2024 mkoani Njombe, ametangaza kukata rufaa kwa Kamati Kuu ya Chadema, akidai kukiukwa kwa taratibu za uchaguzi huo.
Msigwa leo Juni 5, 2024 ameshiriki mkutano katika Kijiji Ughandi, kilichopo jimbo la Singida Kaskazini.
Akihutubia Mchungaji Msigwa amesema matatizo mengi yanayowakumba Watanzania hayatokani na Mungu ila yanasababishwa na fikra finyu za baadhi ya viongozi.
“Tuache kuwa kama chura aliye chini ya kisima anadhani upana wa anga ukubwa wake kama kisima, tokeni kwenye fikra finyu tuende juu tutumie fikra zetu kufanya tunayotaka kujiletea maendeleo,” amesema.
“Chama chetu kinadai Katiba mpya, ni muhimu muungane nasi kuondoa mfumo uliopo. Rais ana mamlaka makubwa ya kuteua na watumishi hao wana nguvu kuliko wanaopigiwa kura na wananchi,” amesema.
Amedai kutokana na ubovu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano, watendaji wa vijiji, kata, wakurugenzi wa halmashauri, wakuu wa wilaya na mikoa wana nguvu kuliko hata madiwani na wabunge wanaochaguliwa na wananchi.
“Ifike hatua turudishe nguvu zetu ikitokea mkurugenzi amekosea basi wananchi tuwe na nguvu ya kumfukuza kazi na siyo kusubiria maagizo kutoka juu. Katiba iliyopo haitoi nguvu kwa wananchi kusimamia kodi zao,” amesema Mchungaji Msigwa
Kwa upande wake, Lissu amesema ni muhimu Watanzania kufikiria kuchagua viongozi wengi kutoka vyama vya upinzani katika uchaguzi ujao ili kumaliza aliodai udhalimu uliotamalaki nchini.
Amesema kuendelea kuwaacha viongozi waliopo, ambao hata wakiingia kwenye vikao vya uamuzi hawajui kuwatetea wananchi ni wazi suluhu ya kupata unafuu wa hali ya maisha haiwezi kupatikana.
“Mkichagua tena viongozi hawa-hawa katika uchaguzi ujao matatizo yataongezeka kwa hiyo kama tunataka suluhu na kupata nafuu ya hali ya maisha jambo la kufanya ni kumalizana nao kupitia kura,” amesema.
“Ni muhimu kuchagua chama tofauti kuondoa mambo magumu, niliwahi kuwa Mbunge Singida Mashariki niliondoa ukandamizaji mwingi, ikiwemo ushuru na tulichokifanya ni kuchagua wenyeviti wa vijiji 11 katika vijiji 101…,” amesema.
Awali, Askofu Maximilian Machumu maarufu Mwanamapinduzi anayeandamana na Lissu katika mikutano hiyo, amesema wananchi wanapaswa kubadilika kwa kutowatumainia viongozi ambao hawana dhamira ya kuwatumikia.
“Ni muhimu mkatumia nguvu yenu ya kura katika uchaguzi unaokuja kwa kuchagua viongozi wanaofaa na kuachana na wanaokuwa madarakani muda mwingi wanajali masilahi yao binafsi,” amesema.