WAALIMU NA WAJASIRIAMALI WAFURAHIA FURSA ZA UWEKEZAJI

Na. Eva Ngowi, WF, Rukwa

Serikali imetoa rai kwa Wananchi kuwekeza fedha zao sehemu sahihi na salama badala ya kuwekeza fedha mahali ambapo pana vihatarishi.

Akiongea katika semina na Wajasiriamali wadogo iliyofanyika katika Soko la SabaSaba kwenye ukumbi wa Mwenyekiti wa Soko hilo mjini Sumbawanga, Afisa Mkuu Mwandamizi Idara ya Uendeshaji wa Sekta ya Fedha, Bw. Salim Kimaro alisema kwa kuwekeza kwenye mifuko kama ya UTT inaruhusu mwananchi mwenye mtaji wa kawaida kuwekeza na kujipatia faida kila mara na kila anapoendelea kuwekeza.

Alisema kuwa uwekezaji salama upo wa aina mbalimbali, mtu anaweza kuwekeza kwa kununua Hisa, Hati Fungani pamoja na kuwekeza katika Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja.

” Tumepata fursa ya kukutana na wajasiriamali hapa sokoni, na kuwapa elimu ya fedha kuhusu masuala mbalimbali kama yalivyoainishwa katika mpango wetu wa utoaji elimu ya fedha au program yetu ya kutoa elimu ya fedha kwa umma. Katika masuala ambayo tumeendelea kusisitiza, pamoja na mambo mengine ni uwekezaji ambao utawasaidia mbali na shughuli zao za biashara ili wapate uhakika wa kupata kipato nje ya biashara ile wanayoifanya moja kwa moja. “Alisema Bw. Kimaro

Bw. Kimaro aliongeza kuwa ni vyema pia wananchi wakawekeza kwenye Hati Fungani za Serikali ambazo unatoa fedha kwa ajili ya kununua hati fungani kwa makubaliano maalum ya umri au muda wa hati fungani husika kama ni miaka mitano, saba, kumi, kumi na tano na kuendelea, na kila miaka ambayo atachagua kuweka hati fungani zake inakuwa na riba yake kulingana na hati fungani husika.

“Ni sehemu ambayo imekuwa ni salama zaidi kwa sababu hakuna athari zinazotokana na uwekezaji wa namna hii, hivyo wananchi wanashauriwa kuwekeza katika hatifungani kama hizo maana ni salama zaidi. Mfumo wake ni kwamba utakapokuwa umewekeza makubaliano yake ni kulipwa riba ambayo italipwa mara mbili kwa mwaka utalipwa kiasi hicho na mwisho wa mkataba wako ambapo kama ni miaka kumi utakapokwisha fedha zako zitarudishwa kama ulivyoziweka”.Alisisitiza Bw. Kimaro.

Kwa upande wa Afisa Elimu ya Watu Wazima katika Shule ya Sekondari Bi. Aggresiana Kilenga, ambaye alihudhuria semina ya Elimu ya Fedha kwa waalimu wa shule ya Msingi na Sekondari iliyofanyika katika kumbi za Manispaa ya Sumbawanga alisema Mafunzo ya Uwekezaji yatamsaidia na kwamba akipata mafao yake atachukua kiasi fulani ili akawekeze kwenye Hati Fungani.

“Mafunzo ya leo nimeelewa yamenisaidia kwa sababu sikuwa na elimu ya uwekezaji kwenye hati fungani ya Serikali kwa hiyo nimevutiwa nayo, na kama nitapewa mafao yangu ya kustaafu maana nakaribia kustaafu naweza nikafikiria kuweka kiasi fulani kwenye hiyo Hati Fungani ya Serikali kwa sababu ni uwekezaji ambao unapata faida kwa mfululizo bila ya kuwa na kikwazo chochote. “Alisema Bi. Kilenga.

Hati Fungani za Serikali hutolewa kwa Umma na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa niaba ya Serikali kupitia Soko la Awali ili kuiwezesha Serikali kupata fedha za kugharamia miradi ya maendeleo. Baada ya mauzo ya awali, Hati Fungani hizo huorodheshwa kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) ambapo Hati Fungani hizo huuzwa na kununuliwa kwa wawekezaji mbalimbali kulingana na nguvu ya Soko.

Related Posts