UJENZI wa ukarabati wa Soko la Kariakoo umefikia asilimia 93 kukamilishwa tayari kuwarejesha wafanyabiashara kwenye soko hilo ambapo hadi sasa hatua kadhaa zimeendelea kuchukuliwa ikiwemo utambuzi na uhakiki wa waliokuwa wafanyabiashara kabla ya janga la moto.
Aidha Valentine amezitaja faida mbalimbali ambazo zitapatikana pale mradi huo utakapokamilika kuwa ni kuongezeka kwa nafasi za biashara kufikia 3,500, ajira zisizo za moja kwa moja zisizopungua 4,000, kuboresha mandhari ya jiji la Dar es Salaam ambalo ni kitovu cha biashara nchini.
Amesema takwimu za shirika la masoko ya kariakoo zinaonesha kuwa sh. 497,773,019.00 madeni ambayo walilimbikiza kwa muda mrefu ambapo madeni hayo yanapaswa kuwa yamelipwa na wafanyabiashara kabla ya kurejea sokoni ili wapate nafasi ya kusajiliwa na mfumo.
Aidha amesema kuwa hadi sasa kiasi cha sh. 15,830,977.71 sawa na asilimia 3 ya deni linalodaiwa kimekusanywa hadi Aprili 2024.
Pamoja na hayo amewataka wafanyabiashara kutimiza wajibu wao wa kisheria wa kulipa deni alilokuwa amelimbikiza kabla ya kusitisha shughuli za biashara Julai 10, 2021 kwenye soko hilo.
“Kwa taarifa hii, Shirika la Masoko ya Kariakoo linapenda kuwakumbusha wafanyabiashara kutumia kipindi hiki kifupi kilichobaki kabla ya ufunguzi rasmi wa soko kukamilisha ulipaji madeni yao hatua itakayoondosha malalamiko na usumbufu wakati wa kuomba nafasi,”. Amesema
Mbali na hayo, Valentine amesema kutokana na maboresho yanayofanyika katika uendeshaji wa biashara katika soko jipya la Kariakoo na maagizo ya Serikali kutumia mifumo ya kielektoniki ili kuleta tija, Shirika litatumia mfumo wa kielektoniki wa TAUSI kutangaza maeneo ya biashara na kukusanya mapato.
“Shirika halitaruhusu mfanyabiashara mwenye deni la awali kupata umiliki wa eneo la kufanya biashara katika Soko la Kariakoo.”Ameeleza Valentine
Hata hivyo amesema Serikali inaendelea kushirikiana na wadau wote wa soko la Kariakoo wakiwemo wafanyabiashara, Mamlaka za usimamizi na udhibiti wa majanga pamoja na kodi kuhakikisha soko litakapoanza kazi linakuwa na viwango vya kimataifa vya usalama ili kuleta ufanisi na tija katika kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Kaimu Meneja Mkuu wa Shirika la masoko ya Kariakoo (KMC), Sigsibert Valentine akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 22, 2024 katika Ofisi za OR- TAMISEMI jijini Dar es Salaam