KESHO Chama cha Soka la Wanawake Mkoa wa Mwanza (WFAMZ) kitafanya uchaguzi mkuu kupata uongozi mpya utakaochaguliwa na wapigakura 12, huku kukiwa na mnyukano mkali ambao umefanya kamati ya uchaguzi huo kutoa onyo kali.
Nafasi zinazogombewa kwenye uchaguzi huo ni mwenyekiti na Sophia Makilagi anatetea kiti chake akikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa Mwenyekiti wa zamani wa chama hicho, Sophia Tigalyoma ambaye uchaguzi uliopita alibwagwa na Makilagi.
Nafasi ya Mjumbe wa mkutano mkuu taifa inawaniwa na Revina Muzawena anayetetea nafasi hiyo akichuana na Johari Ngassa, huku nafasi ya Mjumbe wa kamati tendaji ikiwaniwa na Glory Mbise, Hawa Bajanguo, Flora Gaguti na Elizabeth Nyingi.
Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi huo, Alhaji Majogoro alisema wamebaini uwepo wa mchezo mchafu kwa wapigakura wasiosajiliwa kupachikwa ili wakapige kura na ameonya na kudai wanafanya uthibitisho wa wapigakura hao ili kuondoa udanganyifu.
“Kamati tumefanya ukaguzi wetu tumepata mashaka kwa baadhi ya wapigakura katika usajili wa baadhi ya timu tumeona ni vyema tukathibitisha kwa mamlaka husika ili tupate orodha halisi ya klabu za wanawake zilizosajiliwa,” alisema Majogoro.
“Kwa sababu kuna ujanja unataka kutokea baadhi ya timu kuchomekwa wapige kura jambo ambalo siyo sahihi, tunataka tupate wapigakura halisi wanaokidhi vigezo tukishajiridhisha tutatoa orodha hiyo.”
“Ili tutoe nafasi kwa wagombea waombe kura kwa klabu sahihi, hatutaki kuwa watu ambao wanapitisha watu kwa masilahi yao, tunataka wapigakura halisi wawachague viongozi sahihi,” alisema.