Tetesi za ANC kujiunga na DA zaibua maandamano Afrika Kusini

Johannesburg. Wakati Chama cha African National Congress (ANC) cha Afrika Kusini kikiwa kimejifungia kutafakari kiungane na chama kipi kuunda Serikali, tetesi zimeibuka kuwa chama hicho kinatarajia kuungana na chama cha Democratic Alliance (DA).

Tetesi hizo zimeibua hasira kwa baadhi ya wanachama wa ANC na wameanza maandamano ya kupinga.

Wakati ANC ikiwa njiapanda, muda wa kikatiba wa Bunge kuchagua Rais unaendelea kuyoyoma, kuelekea siku ya mwisho Juni 16, 2024.

Hii ni mara ya kwanza kwa ANC kupata matokeo mabaya kiasi cha kushindwa kuunda Serikali tangu harakati za ukombozi zilizoongozwa na Nelson Mandela zilipokiwezesha kuongoza Serikali mwaka 1994 na kuhitimisha utawala wa makaburu.

Licha ya matokeo mabaya zaidi katika uchaguzi wa Mei 29, ANC inabaki kuwa chama kikubwa zaidi nchini na kitadhibiti viti 159 kati ya 400 katika Bunge jipya la Kitaifa. Matokeo ya uchaguzi yamemweka njiapanda Ramaphosa na chama chake.

Washindani wa karibu wa ANC ni Democratic Alliance (DA) inayounga mkono biashara, yenye viti 87; uMkhonto we Sizwe (MK) inayoongozwa na Rais wa zamani Jacob Zuma, yenye viti 58; na Economic Freedom Fighters (EFF) yenye viti 39.

Baada ya kikao cha Kamati Kuu ya Utendaji ya chama hicho kilichoketi jijini Johannesburg jana Alhamisi Juni 6, 2024, Rais Cyril Ramaphosa alisema ANC imeamua kwamba ushirikiano mpana na nguvu zingine za kisiasa ni chaguo bora zaidi kupeleka nchi hiyo mbele.

“Vyama vya siasa vinapaswa kuungana kujenga mustakabali wa pamoja kwa nchi yetu. Lazima tuchukue hatua kwa haraka kulinda umoja wa kitaifa, amani, utulivu, ukuaji wa uchumi jumuishi, kutokuwa na ubaguzi wa rangi na jinsia,” alisema Ramaphosa alipozunguza na waandishi wa habari.

“Hatutakataza uwezekano wa kufanya kazi na chama chochote, ilimradi ni kwa masilahi ya umma,” alisema Ramaphosa.

Aliongeza kuwa ANC tayari imefanya majadiliano yenye kuungana na EFF, DA, chama kidogo cha Inkatha Freedom Party, National Freedom Party na Patriotic Alliance.

MK ilithibitisha katika taarifa Alhamisi kuwa imekuwa na mawasiliano na ANC na mkutano unatarajiwa hivi karibuni.

Taifa hilo lenye uchumi mkubwa zaidi barani Afrika, limekuwa likiporomoka kwa miaka 10 iliyopita, na ukuaji dhaifu, viwango vya juu vya umaskini na ukosefu wa ajira, miundombinu inayoporomoka na ufisadi wa kisiasa.

“Madhumuni ya serikali ya umoja wa kitaifa lazima kwanza kabisa yashughulikie masuala muhimu ambayo Waafrika Kusini wanataka yashughulikiwe,” Ramaphosa alisema.

Bunge jipya lazima likutane ndani ya wiki mbili baada ya kutangazwa kwa matokeo ya Jumapili na mojawapo ya kazi zake za kwanza ni kumchagua Rais.

Hata hivyo, DA kwa upande wake, iliweka wazi kuwa haitaki kujiunga na Serikali ambayo pia inajumuisha MK au EFF.

Makubaliano yoyote na DA yanaweza kukaribishwa na masoko ya kifedha nchini humo, lakini yatakuwa machungu kwa wafuasi wengi wa ANC, wanaoiona kama chama cha wachache weupe matajiri wa Afrika Kusini.

Waandamanji wamekusanyika nje ya hoteli ambapo mkutano wa NEC ulikuwa unafanyika, wakishikilia mabango yaliyosomeka “DA inataka kuharibu ANC”.

Kwa upande mwingine, makubaliano na EFF au MK, ambayo yanapigania kutaifisha migodi na kuchukua ardhi bila fidia, yangekuwa maarufu zaidi kwa baadhi ya wafuasi wa ANC lakini yanaweza kuathiri uchumi, wamesema wachambuzi.

EFF inayoongozwa na Julius Malema na MK ya Jacob Zuma waliokuwa viongozi wa ANC, hawapatani na Ramaphosa.

Zuma amekuwa akionyesha chuki za waziwazi kwa Ramaphosa, na chama chake kilisema baada ya uchaguzi hakitafanya kazi na “ANC ya Ramaphosa.”

ANC nayo imeweka wazi kuwa haitazungumza na yeyote anayetoa sharti la kujiuzulu kwa Ramaphosa kama hali ya kujiunga na muungano.

Zuma alilazimishwa kuacha urais mwaka 2018 baada ya mfululizo wa kashfa za ufisadi badala yake akachaguliwa Ramaphosa.

Alihukumiwa kifungo jela kwa kudharau Mahakama baada ya kukataa kushiriki katika uchunguzi wa ufisadi, uamuzi uliomzuia kugombea ubunge.

Bado Zuma anabaki kupendwa katika jimbo lake la nyumbani, lililo na watu wengi la KwaZulu-Natal, ambako Polisi wa ziada wamepelekwa wiki hii kudumisha amani ya umma.

Jimbo hilo lilikuwa eneo la machafuko mabaya mwaka 2021 wakati Zuma alipohukumiwa kifungo.

Related Posts