SERIKALI imesema ukomo wa michango kwa wanafunzi wanaojiunga kidato cha tano katika shule za sekondari za serikali ni Sh 80,000 kwa shule za bweni na Sh 50,000 kwa shule za kutwa. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Hayo yamebainishwa leo Ijumaa na Naibu Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Zainab Katimba bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa Konde Mohamed Said Issa.
Mbunge huyo amehoji Serikali ina mpango gani wa kuleta unafuu wa gharama za michango ya kujiunga na masomo ya kidato cha kwanza na cha tano.
Pia katika maswali ya nyongeza Issa, alitaka kufahamu kama Serikali iko tayari kuainisha aina ya michango ambayo imeruhusiwa kuombewa kibali.
Akijibu maswali hilo, Katimba Serikali inatekeleza sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 toleo la 2023 ambalo pamoja na mambo megine inatamka kuwa serikali itahakikisha kuwa elimu ya awali, msingi na sekondari inatolewa bila ada katika mfumo wa umma.
Aidha, amesema waraka wa elimu Na. 3 wa mwaka 2016 kuhusu utekelezaji wa ElimuMsingi bila malipo, unabainisha majukumu ya wadau wote ikiwa ni pamoja na utaratibu wa kuzingatia ili kupata kibali cha mchango wa aina yoyote.
“Ili kuleta unafuu wa gharama za michango, serikali imetoa maelekezo ya kujiunga na kidato cha tano katika shule zote za sekondari za Serikali Tanzania ambapo ukomo wa michango hiyo umebainishwa kuwa shilingi 80,000 kwa shule za bweni na shilingi 50,000 kwa shule za kutwa.
“Aidha, wanafunzi wa kidato cha kwanza wanapokelewa kwa kuzingatia Waraka wa Elimu Na. 3 wa mwaka 2016 wa ElimuMsingi bila ada ambapo wanafunzi hawatikiwi kutoa mchango wowote bila kibali cha waheshimiwa wakuu wa wilaya,” amesema.
Akijibu maswali ya nyongez, Katimba amesema waraka namba tatu umeeleza juu ya utaratibu wa kuomba michango na ni lazima kupata kibali cha mkuu wa wilaya.
Amesema michango hiyo inawezekana ikawa ni ile ya wazazi wenyewe au kupitia kamati za shule, hivyo wazazi wanakubaliana.
Ametoa mfano kuwa wanaweza wakataka kuwe na masomo ya ziada, michango ya uendeshaji wa shule ambapo ukomo umewekwa kwa shule za bweni.
Aidha, Katimba amesisitiza maagizo kwa maofisa elimu na wakuu wa shule, kuwa hawaruhusiwi kuwakataa wanafunzi kwa sababu tu ya kukosa pesa za michango.
Pia amewataka wazazi wa wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano kuwapeleka shule watoto wao hata kama hawajakamilisha michango.