Sababu 5 vigogo kung’oka Simba…Nini hatma ya Mangungu na wenzie!

KWA takribani saa 48 sasa kuna mambo kibao yanaendelea ndani ya Simba. Tajiri Mohamed Dewji ‘MO’ ameingia msituni mwenyewe. Ameamua kufumua kitu kimoja baada ya kingine kwa vitendo katika kuhakikisha Simba inakuwa moto wa kuotea mbali msimu ujao na kurejesha heshima ambayo imepoteza katika misimu mitatu mfululizo iliyopita.

Baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya baada ya Simba kumaliza msimu ikiwa haijatwaa taji lolote kubwa huku ikimaliza katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi, Dewji ameingia kazini kwa kufanya uamuzi mgumu ambao unalenga kuweka mambo kwenye mstari ulionyooka ili timu isiwe na unyonge msimu ujao.

Mwanaspoti linajua kuna sababu tano zilizomfanya Dewji kufanya uamuzi huo;

Pamoja na mambo mengine lakini presha ilikuwa kubwa kwa bodi ya wakurugenzi kutokana na matokeo duni ya Simba uwanjani. Haswa kwa fedheha ya kupigwa nje ndani na Yanga msimu huu.

Hivyo akaanza kwa kuwawajibisha wote walioko ndani ya mamlaka yake ya uteuzi. Kwa kuanzia, Dewji ambaye kwa mujibu wa Jarida la Forbes ndiye mtu tajiri zaidi hapa Tanzania akiwa na utajiri unaofikia Dola 1.8 bilioni (Sh4.7 trilioni) amewapa presha wajumbe wa bodi ya wakurugenzi ya klabu hiyo kujiuzulu kwa kile kinachotajwa kuwa klabu haijaweza kufikia malengo ambayo imejiwekea ya kufanya vizuri kwa msimu wa tatu sasa.

Uamuzi huo umeonekana kupokewa bila hiyana na wajumbe watano kati ya saba ambao wameteuliwa na mwekezaji huyo huku mjumbe mmoja akibakia ambaye ni mwenyekiti wa sasa wa bodi ya wakurugenzi ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’.

Iko hivi. Bodi ya Wakurugenzi Simba ilikuwa ikiundwa na watu 10 kutoka pande mbili yaani upande wa Wanachama na Muwekezaji, Mohammed Dewji ‘Mo’.

Upande wa Mo, aliteua wajumbe watano tu ambao ni Try Again ambaye ni mwenyekiti wa bodi hiyo na Raphael Chageni, Hamza Johari, Zulfikar Chandoo na Rashid Shangazi ndio wamejiuzulu.

Mbunge wa Mlale, Rashid Shangazi ambaye ni mmoja wa wajumbe wa upande wa muwekezaji huyo waliojiuzulu, alisema jana kuwa wameamua kufanya hivyo ili kumpa nafasi Dewji kuingiza sura mpya.

“Nimefanya hivyo kama sehemu ya uwajibikaji kwa namna ambavyo hatukuwa na matokeo mazuri katika takribani misimu hii miwili. Mimi kama kiongozi nimejitathmini nimeona kwamba inawezeka kuna mahali hatukufanya vizuri sana basi uungwana ni kupisha ili mwenyekiti na mwekezaji wetu aweze kutengeneza safu upya ya bodi ambayo itakwenda kuisimamia Simba SC iweze kuwa klabum irudishe utimamu wake katika kuchukua vikombe.

“Neno moja kwa wanachama, Uongozi ni kupokezana na uongozi unahitaji mshikamano na nguvu ya pamoja. Wasiiache timu, waendelee kuisapoti wakati wote. Haswa kipindi hiki ambacho tupo katika mapitio. Sisi tumewajibika ili tuweze kujipanga upya lakini tutakuwa na mchango ambao tutaendelea kuutoa kwenye timu kwa kadri inavyohitajika,” alisema Shangazi.

Pamoja na kwamba Dewji aliwateua mwenyewe wajumbe hao, uamuzi wa kuwaomba wajiuzulu ameuchukua ili kutokiuka katiba ya klabu hiyo ambayo inafafanua kuwa mjumbe wa bodi atakoma kutumikia nafasi yake ikiwa mambo manne yatatokea.

“Mjumbe wa bodi ya wakurugenzi aliyechaguliwa na kuteuliwa kwa mujibu wa ibara ya 27 ya katiba hii atakoma kuwa mjumbe wa bodi ya wakurugenzi iwapo atatenda au kufanya mojawapo ya mambo yafuatayo.

(a) Kujiuzulu kwa maandishi na kuwasilisha barua yake ya kujiuzulu kwa bodi ya wakurugenzi. (b) Hatohudhuria mikutano minne mfululizo ya kawaida ya bodi ya wakurugenzi. (c) Anashindwa kutekeleza majukumu ya mjumbe kutokana na kuumwa au sababu nyingine yoyote kwa kipindi cha miezi 12 mfululizo,” inafafanua ibara ya 29 ya katiba hiyo.

UPANDE WA MANGUNGU ITAKUWAJE?

Presha hiyo ya kujiuzulu inawakabili pia wajumbe wa bodi ya wakurugenzi akiwemo Mwenyekiti, Murtaza Mangungu ambao hawakuteuliwa na Dewji lakini kutokana na kutokuwa na mamlaka ya kikatiba, mpira huo umeachwa kwa wanachama kuamua wakati wa mkutano mkuu wa klabu hiyo.

Upande huu wanachama walikuwa  Seif Muba, Asha Baraka, Issa Masoud, Rodney Chiduo na Seleman Haroub na Mangungu.

Habari za ndani ambazo Mwanaspoti imezipata jana jioni ni kwamba huenda kukaibuka ombi la mkutano mkuu wa dharura muda wowote wiki ijayo kwani kuna baadhi wanashinikiza hilo kwenye mitandao ya kijamii na hata klabuni jana ilikuwa miongoni mwa mijadala gumzo.

Mwanaspoti linajua MO ameamua kuingia mwenyewe kusimamia usajili mpya. Hivyo hakutaka yeyote kwenye jopo ajihusishe tena na zoezi hilo kwavile mambo hayaendi. 

Jambo la pili ambalo Dewji ameamua kuwa mstari wa mbele ni kushiriki kwa ukaribu mchakato wa usajili wa nyota wapya ambao wataitumikia klabu hiyo ikiripotiwa kwamba hakuridhishwa na namna timu hiyo ilivyokuwa ikiendesha zoezi hilo kwa miaka ya hivi karibuni.

Na katika kuhakikisha hilo linafanyika kwa umakini na ubora wa hali ya juu, Dewji ameamua kuwaongeza watu wanne wazoefu wa masuala ya usajili kusimamia zoezi hilo ambao Simba imeshawarudisha, Crecensius Magori, Mulamu Nghambi, Kassim Dewji na Sued Mkwabi.

Ikumbukwe wakati Magori akiwa mtendaji mkuu wa klabu hiyo ndio aliifanya iwe na kikosi tishio akisajili nyota kama Clatous Chama, Luis Miquissone, Meddie Kagere na Pascal Wawa.

Meneja habari na mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally aliwahi kunukuliwa akithibitisha mchakato wa usajili ni zoezi litakalosimamiwa na Dewji mwenyewe.

”Fedha yote ya usajili ya msimu ujao atatoa Dewji na mzigo ambao umetengwa kwa ajili ya usajili ni mkubwa. Niwaambie, Mo tunaye sana na tunatamba naye, usajili huu unaokuja atausimamia mwenyewe kwa asilimia mia moja.

“Kwa hiyo wanachama na mshabiki msiwe na wasiwasi, atasimama mwenyewe kwa miguu miwili kuhakikisha wachezaji bora na wa gharama wanatua kwenye klabu hii, mateso, manung’uniko, masononeko sasa basi,” alisema Ally.

Kwa kuanzia, Simba tayari imefanikisha usajili wa kiungo Yusuph Kagoma kutoka Singida Fountain Gate na beki Lameck Lawi wa Coastal Union.

MO pia ameamua kupitisha fagio la chuma kwa wachezaji wengi ambao wameonekana umri umewatupa mkono akizuia kuongezewa mikataba mipya kama ambavyo ametaka wale walioonyesha viwango vya chini kuonyesha mlango wa kutokea.

Miongoni mwa wachezaji ambao Bilionea huo ameamua wasipate mikataba mipya ni Saido Ntibazonkiza, John Bocco, Shomari Kapombe na Clatous Chama.

Kingine kilichomsukuma Dewji kufanya maamuzi ni baada ya kuona zoezi la kuongeza wanachama limekwama. Anataka mchakato wa usajili wa wanachama urudishwe kwa haraka ili kuiwezesha klabu kuingiza fedha kupitia ada za usajili lakini pia iongeze thamani na ukubwa wake.

Juzi Alhamisi, hilo lilianza kufanyiwa kazi kwa klabu hiyo ilitangaza ajira ya mkurugenzi wa wanachama na mashabiki.

Ni siri kubwa lakini Mwanaspoti linajua Barbara Gonzales anamrudisha kama Mwenyekiti wa Bodi.Inaelezwa inasubiriwa Try Again ajiuzulu kisha Barbara akaimu nafasi ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi na hapo baadae atapigiwa kura na wajumbe kuidhinishwa.

Barbara atafanya kazi na wajumbe wapya watakaoteuliwa na Mo, sambamba na wale wa upande wa Wanachama na sekretarieti nzima ya Simba.

Sambamba na Barbara maeneo mengine yatakuwa na mabadiliko makubwa, muda wowote Mtendaji Mkuu, Imani Kajula atabwaga manyanga nafasi yake itakapopata mtu kwani inadaiwa tayari ameshamalizana na viongozi na mchakato ulishaanza.

Za ndaani kabisa aliyewahi kuwa meneja wa Simba kwa muda mrefu,  Patrick Rweyemamu atarejea kwenye majukumu yake.

Meneja huyo kipenzi cha Wanasimba kwa sasa ni mkuu wa maendeleo ya vijana katika timu hiyo lakini Mwanaspoti linajua muda wowote anaweza kurejea kwenye umeneja kuchukua nafasi ya Mkenya Mikael Igendia anayeachana na timu hiyo.

Rweyemamu ni miongoni mwa watu wenye ushawishi mkubwa ndani ya Simba lakini pia amehusika katika mafanikio ya timu hiyo kwa zaidi ya miaka 15 sasa.

Wakati hayo yakiendelea baadhi ya wadau mitandaoni wameibuka na hisia tofauti wakihisi ni miongoni mwa hatua za kuondoka ndani ya klabu hiyo kwa tajiri Mo.

Wadau hao tofauti wanaamini Mo amewataka wajumbe aliowateua yeye wajiuzulu ili apate nafasi nzuri ya kuachia ngazi kutokana na kile anachokitaja mara kwa mara kuwa anapata hasara kupitia Simba.

Ikumbukwe bado mchakato wa mabadiliko wa Simba haujakamilika. Mchakato huo ni ule utakaorasimisha Muwekezaji/Wawekezaji kumiliki asilimia 49 ya hisa za timu hiyo huku Wanachama wakimiliki asilimia 51, jambo ambalo limechukua muda mrefu.

Hata hivyo, Mwanaspoti limepenyezewa taarifa, tajiri huyo bado yupo Msimbazi na kwa sasa anasimamia mwenyewe mambo mengi ya timu hususani usajili. Mwanaspoti lilimtafuta Try Again akasema; “Sipo Tanzania, ni lazima nirudi ofisini ili nifanye mambo ya kiofisi, kwa sasa siwezi kuzungumza jambo lolote.”

Aliyekuwa mfadhili wa Simba na ndugu wa Mo, Azzim Dewji alipotafutwa kuzungumzia hilo alijibu kwa ufupi “Naomba tusubiri kidogo tafadhali.”

Related Posts