Kiraka Azam huyoo anukia Al Hilal

BAADA ya kumaliza mkataba wa kuitumikia Azam FC, kiraka Edward Charles Manyama anatarajia kutimkia Al Hilal ya Sudan tayari kwa kukipiga huko msimu ujao.

Manyama juzi kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook aliwaaga mashabiki, wachezaji na viongozi wa timu hiyo akithibitisha kumaliza mkataba na timu hiyo aliyoitumikia kwa mkataba wa miaka miwili.

Chanzo cha kuaminikia kutoka kwa rafiki wake wa karibu kililiambia Mwanaspoti kuwa staa huyo licha ya mkataba wake uongozi wa timu hiyo ulijaribu kumshawishi abaki lakini mpango wake ulikuwa ni kuondoka.

“Kamaliza mkataba na Azam na alikuwa na ofa ya ndani Singida Fountain Gate na nje Al Hilal ya Sudan timu ambayo ilituma ofa wakati wa dirisha dogo lakini walikwama kutokana na mchezaji huyo kuwa na mkataba,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;

“Timu aliyoipa kipaumbele ni Al Hilal ambayo ilionyesha nia ya kumuhitaji tangu dirisha dogo, kilichokwamisha ni mkataba aliokuwa amebakiza na waajiri wake wa zamani Azam. Ni wazi sasa anatimka nchini.” 

Mwanaspoti lilifanya jitihada za kumtafuta kiraka huyo ambaye alithibitisha kumaliza mkataba na Azam, huku akifunguka alikuwa na maisha mazuri ndani ya timu hiyo kilichomuondoa ni kujaribu changamoto nyingine nje ya timu hiyo.

“Mimi ni mchezaji, kupokea ofa hasa kipindi hiki cha usajili ni suala la kawaida na nimeamua kuondoka Azam timu ambayo imenilea vizuri nimeishi nao vizuri kuanzia benchi la ufundi, wachezaji wenzangu hadi viongozi, lakini nafikiri huu ni wakati wangu kuondoka,” alisema Manyama na kuongeza;

“Nimeondoka Azam ni wazi kuna timu naenda lakini sio wakati sahihi kusema ni wapi, kwa sasa nafikiri naomba muda ili mambo yakienda sawa juu ya timu gani nitacheza kati ya hizo ulizozitaja au nje ya hizo kila mtu atafahamu.” 

Manyama alimalizia kwa kusema kuwa anafuatilia hati yake ya kusafiria na akikamilisha hilo anatoa nafasi ya kufanya mahojiano na Mwanaspoti.
 

Related Posts