Kiungo Azam atajwa Yanga, mchongo mzima upo hivi

SIKU chache baada ya sintofahamu ya kukosa saini ya kiungo, Yusuph Kagoma, mabosi wa Yanga wapo kwenye mchakato wa kuibomoa Azam FC kwa kumnasa kiungo fundi, Adolf Mtasingwa aliyebakiza mkataba wa miezi sita kuitumikia timu hiyo.

Mwanaspoti linafahamu, Yanga kwa usiri mkubwa imeanza mazungumzo na kiungo huyo aliyekuzwa timu ya Vijana ya Azam aliyeng’ara katika mechi ya Fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Yanga akichuana vikali na mastaa wa Yanga, Khalid Aucho, Mudathir Yahya na baada Jonas Mkude.

Taarifa zaidi zinasema Yanga imepata mzuka wa kumbeba kiungo huyo wanayeona anaweza kuwa mbadala sahihi wa Aucho, huku ikielezwa amegoma kuongeza mkataba mpya na wana lambalamba hao.
Nyota huyo aliyewahi kukichezea kikosi hicho akiwa akademi amerejea nchini baada ya mkataba wake kumalizika na uongozi wa Azam FC kumpa mkataba wa mwaka mmoja.

Chanzo cha kuaminika kutoka kwa rafiki wa karibu wa mchezaji huyo kimeliambia Mwanaspoti, Mtasigwa amechomoa kusalia Chamazi baada ya kupata ofa kadhaa ikiwamo ya Yanga, wakati mkataba na klabu hiyo ukibakiza miezi michache kabla ya kumalizika.

“Mtasingwa kabakiza miezi sita tu alisaini mwaka mmoja kuitumikia Azam, kwani hawakuwa na imani naye kutokana na kutokumfuatilia akiwaVolsungur IF ya Iceland baada ya kuwavutia sasa wanapambana kumwongeza mkataba mpya, lakini naye hajaonyesha nia ya kubaki kutokana na kupokea ofa kubwa,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;

“Amepokea ofa kutoka Yanga na wameonyesha nia ya kumpa dau kubwa ambalo limemchanganya nyota huyo wa Kitanzania ambaye amekuzwa katika misingi ya mpira kutokana na kupita kwenye vituo vingi vya kufundisha mpira.” 

Mwanaspoti lilimtafuta kiungo huyo aliyeungana na kikosi cha  Taifa Stars kilichoenda Zambia kucheza na wenyeji katika mechi ya kuwania fainali za Kombe la Dunia 2026 na kusisitiza yeye bado ni mchezaji wa Azam FC, hizo taarifa za kuwindwa na Yanga hawezi kuzungumzia kwa sasa.

“Mimi bado ni mchezaji wa Azam FC, kuhusu mambo ya kupokea ofa kutoka timu zinazoshiriki Ligi Kuu zikihitaji huduma yangu nafikiri sio swali sahihi kwangu, mimi kazi yangu ni kucheza tu,” alisema Mtasigwa na kuongeza;

“Juu ya mkataba niliobakiza Azam FC ni ishu ambayo ipo wazi unaangalia taarifa za kusaini mkataba wangu hadi sasa nitakuwa nimebakiza muda gani? Lakini hadi sasa mie bado ni mchezaji wa timu hiyo na kama kutakuwa na jipya mtafahamishwa rasmi.”

Endapo Yanga itafanikiwa kumpata kiungo huyo itakuwa imepata mchezaji ambaye atatoa changamoto kwa kiungo Khalid Aucho ambaye amekuwa panga pangua kikosi cha timu hiyo akisaidiana na Jonas Mkude, Mudathir ambaye amekuwa akicheza nane na sita sambamba na Sure Boy.

Mbali na kuichezea Volsungur IF ila timu nyingine alizochezea kiungo huyo ni KR Reykjavik na Keflavík IF zote za Iceland.

Related Posts