Unguja. Wakati bajeti ya Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi ikipitishwa, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamesema bado hawajaona mkakati madhubuti wa kutekeleza sera ya uchumi wa buluu.
Bajeti hiyo ya Sh66 bilioni imepitishwa na Baraza Juni 8, 2024 ikiwa na vipaumbele 12.
Mwakilishi wa Pandani, Profesa Omar Fakih Hamad amesema wizara hiyo ndiyo msingi wa sera ya uchumi wa buluu na kubeba sekta nyingi, lakini hawajaona mafanikio makubwa yanayopatikana kutokana na kutengewa fedha kidogo katika programu zake.
Amesema programu ya uvuvi na ufugaji mwaka 2023/24 iliombewa Sh47.5 bilioni lakini mpaka Machi mwaka huu imeipata Sh4 bilioni, sawa na asilimia tisa.
Programu ya utafiti na uvuvi mwaka 2023/24 iliombewa Sh5 bilioni lakini mpaka Machi imeingiziwa Sh224 milioni sawa na asilimia nne, huku programu ya maendeleo ya uvuvi iliyoombewa Sh54 bilioni ikiingiziwa Sh4 bilioni sawa na asilimia nane.
“Ukiangalia mwendo huu, bado kuna kazi kubwa ya kufanya, nimeshangaa kuona kuna baadhi ya wawakilishi wanapongeza lakini kwa uhalisia wizara hii imeshindwa,” amesema.
Mwakilishi huyo amesema iwapo Serikali imeshindwa kuisimamia wizara hiyo ni vyema ikaiondoa.
Mwakilishi wa Fuoni, Yussuf Hassan Iddi amesema kinachotakiwa ni kuongeza jitihada kuhakikisha wizara hiyo inatekeleza mipango kama ambavyo Serikali inataka.
Akihitimisha hoja za wawakilishi hao, waziri mwenye dhamana na wizara hiyo, Shaaban Ali Othman amesema licha ya changamoto wanazokabiliana nazo ikiwa ni pamoja na watendaji wachache, wanahakikisha wanatekeleza yanayotakiwa.
Amesema baada ya kupitishiwa bajeti wamejipanga kuhakikisha vipaumbele vyao vya kukuza uvuvi vinafanikiwa.
Ametaja miongoni mwa mafanikio ni kuongezeka kwa kiwango cha uzalishaji wa samaki kutoka tani 61,794 wenye thamani ya Sh391.37 bilioni kwa mwaka 2022 hadi kufikia tani 80,085 wenye thamani ya Sh569.07 bilioni kwa mwaka 2023 sawa na ongezeko la asilimia 29.5.
Vilevile uzalishaji wa mwani umeongezeka kutoka tani 12,594 zenye thamani ya Sh10 bilioni kwa mwaka 2022 hadi kufikia tani 16,653 zenye thamani ya Sh16 bilioni kwa mwaka 2023 sawa na ongezeko la asilimia 32.2.