Arusha. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Arusha imekamata kiwanda bubu kilichokuwa kinatengeneza pombe kali kinyume na sheria ambazo pia zinadaiwa kuwa na stempu za kodi za kughushi, huku mwenyekiti wa mtaa akibaki na mshangao.
Kwa mujibu wa ukaguzi wa awali uliofanywa na maofisa wa mamlaka hiyo, stempu nyingine zimekutwa kwenye kiwanda bubu hicho zikiwa na jina la kampuni nyingine.
Akizungumza leo Juni 9, 2024, Meneja Ukaguzi na Upelelezi wa TRA Kanda ya Kaskazini, Todi Beyanga amesema kiwanda hicho kinapatikana katika kata ya Sakina na hadi sasa wanamshikilia mtu mmoja aliyekutwa katika kiwanda hicho kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Amesema wataalamu wa mamlaka hiyo kwa kushirikiana na vyombo vya dola wameanza uchunguzi kumbaini mmiliki wa kiwanda hicho ili achukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria.
“Hii ni shughuli endelevu na tumeweza kubaini kiwanda bubu kinachotengeneza pombe aina ya Gin inayoitwa Game Men na tumebaini huyu mtu amekuwa akizalisha pombe bila kuzingatia taratibu na sheria, kuna hizi katoni 546 ambazo hazijabandikwa hata stika.
“Lakini vilevile kuna katoni tisa zenye stika lakini hizo stika hazina uhusiano wowote na kampuni hii lakini mbali zaidi tumebaini kuna lita 500 za spirit ambazo ziko katika hatua za kuzalisha hii pombe,” ameongeza meneja huyo.
Amesema wanaendelea na uchunguzi katika maeneo mbalimbali jijini Arusha ili kubaini endapo kuna watu wameanzisha viwanda na wanazalisha bidhaa bila kuzingatia sheria na taratibu.
Meneja Msaidizi Huduma kwa Mlipakodi – TRA Arusha, Peter Jackson amesema lengo la ukaguzi huo endelevu ni kuhakikisha serikali haipotezi mapato pamoja na kuwalinda wananchi ili waweze kutumia bidhaa zilizozalishwa kwa ubora unaotakiwa.
Amesema kwa mujibu wa taratibu, mtu akishapata namba ya mlipakodi na anataka kuzalisha bidhaa anapaswa kuanzia kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ambapo atapewa kibali, kisha Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ambao watajiridhisha kama bidhaa inayozalishwa inafaa kwa matumizi.
“Akishapata kibali TBS, sisi tunampa leseni, sasa mhusika huyu hapa hana leseni na sisi hatumtambui. Tuliweza kukibaini kiwanda hiki baada ya timu yetu kukuta bidhaa hizi mitaani zikiwa na stempu feki,” amesema.
“Hadi sasa tunamshikilia mtu mmoja, atatusaidia kumpata mhusika mwenye kiwanda na hatujui amekuwa akifanya biashara hii kwa muda gani, tunachunguza hizi stempu feki wamezipataje na wamezipata wapi,” ameongeza.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Maeriva ambapo kiwanda hicho kimekutwa, Innocent Loda amesema hajawahi kufahamu kama kiwanda hicho kinatengeneza pombe na kwamba alikuwa anajua kinatengeneza sabuni.
“Kwa kweli hiki kiwanda sikifahamu, nilikuwa najua ni kiwanda cha kutengeneza sabuni na tulishawahi kukitembelea, nimeshangaa leo kinatengeneza pombe, kwa mara ya kwanza ndiyo nimeona leo kwani nilishajiridhisha walikuwa wanatengeneza sabuni,” amesema.