Chanda hakinenepi siku ya kuvishwa pete

Wanasema mbuzi hanenepi siku ya mnada. Kama hukumlisha vizuri pale mwanzoni, usitegemee awe na afya njema iwapo utamlazimisha kula ili anenepe wakati wa kwenda sokoni. 

Utaingia hasara kwani atakula misosi ambayo huwezi kumudu gharama zake hata ukijitoa outing, lakini kamwe hutoweza kuongeza thamani yake kiafya. Na utakapompeleka sokoni atakuwa ni yuleyule ambaye hukumpa chakula bora.

Lakini huwezi kuamini kwamba wakati ule tulipokuwa wadogo, hakuna aliyepelekwa dukani akakosa saizi ya viatu vyake. Wakati ule kulikuwa maduka ya kampuni ya Bora iliyokuwa maarufu kwa uuzaji wa viatu. Wazazi walipendelea kutununulia viatu aina ya Safari Buti (wenyewe tukiviita “wembe”). Viatu hivi vilikuwa vya ngozi imara hivyo hawakuwa na haja ya kununua jozi mara kwa mara.

Kwetu viatu hivi vilikuwa na maana zaidi; kwanza vilikuwa ni mkataba; utamaliza navyo shule bila kuchakaa. Ungeweza kuchezea mpira na hata ungependa kupigia mawe bila kuumia au viatu kuchanika. Pili usingelazimika kuvifua wala kupiga kiwi, na tatu wenzako wasingekuchokoza kwa kuuogopa wembe. Ungempiga nacho ugokoni ni lazima angechanika. Ndiyo maana tuliviita wembe.

Lakini upatikanaji wake haukuwa rahisi. Vilitengenezwa kwa uchache na kusambazwa kwenye maduka yao yaliyokuwepo kwenye kila kona ya Jiji. Kila duka liliambulia takribani jozi kumi au pungufu ya hizo.

Wazazi wakiambatana na watoto wao walilazimika kusimama kwenye msururu nje ya duka wakingojea zamu yao ya kuhudumiwa.Humo ndani mtoto angepimwa urefu wa unyayo wake na kununuliwa viatu vilivyomzidi kidogo, hivyo hata kama angerefuka isingelikuwa taabu. 
Lakini kama nilivyosema hakuna mtoto aliyekosa saizi ya kiatu maana hata kama vilimbana angekunja vidole ili vimtoshe. Fikiria umeisaka ndoa kwa udi na uvumba, halafu mchumba anapokuja kukuvisha pete kidole kinakataa ati kimenenepa. Hakyanani utakimenya!

Kwa wale ambao hawakusoma simulizi hii, Sinderera alipendwa na mtoto wa Mfalme aliyekutana naye kwenye sherehe. Akamtoroka usiku lakini kwa bahati mbaya kiatu chake kilimvuka, watumishi wa Mfalme wakawa wakimsaka mji mzima kwa kujaribisha kile kiatu kwenye miguu ya wadada wote. Hakuna kiliyemtosha, na ndipo wadada hao walipokata miguu kukilazimisha.

Hivi sasa wakati tukielekea kwenye Uchaguzi Mkuu, tunaona jinsi viongozi wetu wanavyolazimika kurudi kwenye majimbo waliyoyasahau tangu wakati wa kampeni za uchaguzi uliopita. Huu ndio wakati wao wa kujua matatizo ya majimboni, na pengine kuyatatua kabla mhula unaofuata haujaingia.

Tanzania kuna mambo ya ajabu sana hivi sasa. Watu wake wanatafsiri kila kitu kuwa pesa: Siasa, dini, maradhi, misiba, maneno, yaani kila kitu! Ushindani wa miaka hii kwenye siasa za Kibongo upo kwenye fedha badala ya uwajibikaji. Watu wanaacha taaluma walizosomea, wanauza kila wanachomiliki na kuwekeza kwenye siasa wakiamini kwamba siasa italipa mara nyingi zaidi.

Watafutaji wanahangaika kutafuta mapungufu ili kukandamizia misumari humo. Waliokwisha kupata wanaendeleza hadithi isiyoisha. Ushaisikia hii: “Sisimizi aliingia kwenye nyumba ya Mfalme. Alitembea hapa na pale hadi akaingia jikoni.

“Akaokota kidonge cha sukari chini ya gunia. Akalipeleka kwenye shimo lake. Huko wenzake walimpokea kwa shangwe, akawaelezea jinsi alivyofika pale kwa mfalme na kukuta gunia la sukari lililotoboka chini. Wakatoka kwa pamoja kumfuata sisimizi huyo.

Akachukua kidonge cha pili, na aliyemfuata akaokota kidonge chake cha kwanza. Mwingine naye akaokota cha kwake, na mwingine aliyemfuata akaokota…”
Hadithi hii haiishii hapa na wala haina mwisho. Itaendelea hadi pale gunia litakapokwisha na watakapogundua gunia lingine. Utaisikiliza hadi utalala, na ukiamka utakuta tamthilia ingali ikiendelea.

Unaweza kumfananisha kiongozi anayekumbuka jimbo wakati wa kampeni na mtoto anayelazimisha kiatu kisichomtosha. Maana kama alishindwa kulikumbuka jimbo lake kwa takribani miaka minne anawezaje kulikumbuka katika majuma machache kabla ya uchaguzi unaofuata?

Lakini bahati yao ni kwamba wanakutana na wapiga kura waliokwisha kusahau siasa. Watu wenye njaa na ambao ukiwatajia maendeleo unawatia usingizi. Kitu pekee kinachoweza kuwaamsha ni noti nyekundu.

Wakati wenzetu wana wapiga kura makini wengi kuliko wale wasiojielewa, kwetu ni tofauti kwani uongo ulishageuzwa kuwa ukweli. Ukisema “ndiyo” unaeleweka kinyume chake. , ukimsalimia “mambo vipi?” akakujibu “Mambo poa! Baridi barafu! Kama Ulaya!” wakati mtu mwenyewe hajala toka asubuhi, anaumwa na hana hela.

Lakini ukikutana na majibu ya “Hali yangu dhoofu il-hali” ujue huyo hajambo.

Related Posts