CUF yajipanga kudai Katiba mpya, Tume Huru ya Uchaguzi

Dar es Salaam. Chama cha Wananchi (CUF) kimesema wakati Taifa likielekea kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, kinatarajia kufanya mazungumzo na vyama vingine vya siasa kuhusu suala la Katiba mpya na Tume Huru ya Uchaguzi.

Uamuzi huo wa CUF umechochewa na madai kwamba miswada iliyopitishwa na Bunge na kusainiwa na Rais kuwa sheria, ni danganya toto kwa kuwa maoni ya wananchi pamoja na wadau mbalimbali wa siasa yalipuuzwa.

Februari 2024, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha miswada mitatu ambayo ni Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani na Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa.

Miswada hiyo mitatu ilipitishwa mara baada ya kujadiliwa na wabunge katika mkutano wa 14 wa Bunge jijini Dodoma Februari 02, 2024 ambapo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama alitoa ufafanuzi kuhusu hoja za wabunge zilizowasilishwa wakati wa majadiliano ya miswada ya sheria ya uchaguzi.

Akizungumza na wanahabari leo Jumapili Juni 9, 2024 kuhusu maazimio ya Baraza Kuu la chama hicho lililokutana Juni 3 na 4, 2024, mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba amesema maoni mengi yamepuuzwa ikiwemo kufanyia marekebisho Katiba iliyopo.

“Ngoma itakayopigwa ndio tutakayoicheza, kama wananchi tunapaswa kufahamu tuna vyama 19 vya siasa wakati tunafanya mazungumzo na vyama vingine tunapaswa kuwa makini na kuhimiza wananchi kujiandikisha,”amesema Lipumba.

Amesema mabadiliko waliyoyategemea hayajapatikana, ni lazima kuwa macho na kufanya amshaamsha ya nganari kinoma wakati wa kuelekea kwenye uchaguzi.

“Hali inayoendelea sasa hakuna sheria yoyote iliyotungwa na Bunge, Tume huru kusimamia uchaguzi wa Serikali za mitaa, sheria hizi hazijabadilisha kitu, tutaendekea na utaratibu kama ulivyo,” amesema.

Profesa Lipumba ambaye pia ni mchumi, amesema sheria hizo ni danganya toto kwa kuwa bado zinampa Rais mamlaka ya kufanya uteuzi wa mwenyekiti na makamu mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi.

Amebainisha kuwa tayari Rais ameshateua mwenyekiti na makamu wake ambao wataendelea kufanya kazi hadi hapo muda wao utakapomalizika.

“Hakuna mjumbe yoyote atakayeteuliwa kabla ya mwaka 2025, Rais alishateua mwenyekiti na makamu wake ambao watamaliza muda wao Septemba 2026,” amesema.

Miongoni mwa mambo ambayo CUF kimekuwa kikihitaji ni pamoja na marekebisho ya Katiba, na msingi wa mapendekezo hayo ni kuweka mazingira mazuri ya kisheria.

Jambo linguine, ni wakurugenzi wa halmashauri kutosimamia uchaguzi kwa madai kwamba sio waadilifu, wakiitaka Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kuajiri watumishi watakaokuwa wasimamizi na sio wakurugenzi wanaoteuliwa na Rais.

Pia, CUF kinataka watumishi watakaoteuliwa wawepo wa kudumu kwa ngazi ya halmashauri, wakati pia kikipendekeza kura za urais, kufikia zaidi ya asilimia 50 na kuwe na mwanya wa matokeo yake kupingwa mahakamani.

Kauli hiyo ya CUF imeungwa mkono na baadhi ya vyama ikiwemo Chadema ambapo Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje Chadema, John Mrema amesema chama hicho kipo tayari kushirikiana na vyama vingine kupigania mabadiliko.

Amesema sheria zilizopitishwa bado ziko vilevile na kilichobadilika ni jina tu. “Kwenye utendaji na utekelezaji umebaki vilevile sheria hizo bado ni danganya toto, kwa walio tayari tutashirikiana kudai haki,” amesema Mrema.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Doyo Hassan Doyo amesema hawawezi kushiriki mambo ya watu wengine kwa kuwa sasa wanajipanga kwa ajili ya uchaguzi.

Amefafanua kuwa wametoka kwenye kulalamika na kwenda kwenye sheria, hivyo hawawezi kutafuna wakati wa kupiga mluzi.

Naibu Katibu Mkuu wa Chaumma Bara, Eugene Kabendera amesema suala hilo ni msimamo mzuri na imekuwa ni kiu ya wananchi kwa muda mrefu.

Amesema ni wakati sasa wa kuwa kitu kimoja, hata hivyo chama hicho nacho kiko mbioni kutangaza msimamo na kutoa maoni juu ya suala hilo kuelekea uchaguzi.

“Tumebakiza siku chache kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa, tulitarajia uchaguzi utasimamiwa na tume huru lakini cha kushangaza tunaambiwa Tamisemi wanaandaa kanuni,” amesema Kabendera.

Related Posts