Dar es Salaam. Tamasha la Kimataifa la Utamaduni na Utalii Kanda ya Ziwa lililozinduliwa Dar es Salaam kwa lengo la kuwafikia washiriki wengi zaidi, litafanyika kuanzia Julai 5 hadi Julai 7 mwaka huu Bariadi mkoani Simiyu.
Uzinduzi huo uliofanywa na Kampuni ya Kilimanjaro One Travel and Tours ulihudhuriwa na wadau mbalimbali likiwamo Baraza la Sanaa Tanzania (Basata), Bodi ya Utalii Tanzania na wadau wa utamaduni kutoka Bariadi mkoani Simiyu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam Ijumaa Juni 7 2024 Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Kilimanjaro One Travel and Tours, Christina Emmanuel amesema hii ni mara ya kwanza kwa kampuni hiyo inayojihusisha na masuala ya utalii na utamaduni kuandaa tamasha hilo litakalokuwa na muitikio mkubwa kwa wakazi wa Simiyu na mikoa ya jirani.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Kilimanjaro One Travel And Tours, Christina Emmanuel, akizungumza wakati wa uzinduzi wa Tamasha la Utalii na Utamaduni Kanda ya Ziwa (Lake Zone Cultural and Tourism Festival), jijini Dar es Salaam. Kutoka kulia ni Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Mohamed Hatibu, Mkurugenzi wa Ukaguzi na Maendeleo ya Sanaa kutoka Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Edward Buganga na Ofisa Masoko kutoka Bodi ya Utalii Tanzania, Nassor Garamatatu.
“Tamasha hili linatarajiwa kufanyika mwezi wa saba kwa siku tatu mfulululizo Julai 5, 6 na kilele chake kitakuwa Julai 7; pamoja na mambo mengine tunategemea kuwa na maonyesho mbalimbali ya kiutamaduni na utalii katika Uwanja wa Halmashauri na kuwavutia washiriki na watazamaji takribani 7000 kwa siku hizo tatu,” amesema Christina.
Amesema tamasha litakuwa na vionjo mbalimbali ikiwamo ngoma inayohusisha makabila ya Wagika na Wagulu, maonyesho, michezo mbalimbali na vyakula.
Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Mohamed Hatibu ametoa wito kwa wafanyabiashara, kampuni, taasisi na mashirika kujitokeza na kuunga mkono tamasha hilo ikiwa ni njia mojawapo kuiunga mkono Serikali katika kuutangaza utamaduni na utalii wa Simiyu.
“Tumejiandaa vizuri na tuna uhakika tamasha hili litafanikiwa na litakuwa kila mwaka,” amesema Hatibu na kuongeza kuwa linatarajiwa kuwavutia watalii kutoka ndani na nje ya nchi.
Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji na Maendeleo ya Sanaa wa Basata, Edward Buganga amewasifu waandaaji wa tamasha hilo kwa kuendeleza utamaduni na utalii nchini, huku akitoa wito kwa wadau wengine kuliunga mkono tamasha hilo kwa hali na mali.
“Ni tamasha kubwa la aina yake ambalo sisi kama Watanzania tunapaswa kujivunia kuwa hili ni tamasha la kwetu kwa maendeleo ya utamaduni na utalii wetu,”amesema Buganga na kusisitiza kuwa Basata itatoa ushirikiano mkubwa kwa waandaaji ili tamasha hilo lifanyike kwa ufanisi.
Ofisa Masoko wa Bodi ya Utalii Tanzania, Nassor Garamatatu ameipongeza Kilimanjaro One Travel and Tours kwa kuona umuhimu wa kuunganisha utalii na utamaduni akisema haviwezi kutenganishwa.
“Sasa hivi sisi kama bodi tumejikita sana katika kutangaza utalii wa utamaduni, ndio maana tupo tayari kuliunga mkono tamasha hili ili tutangaze utamaduni na vivutio vya utalii kwa Mkoa wa Simiyu,” amesema Garamatatu.