KWA muda mrefu baadhi ya wadadisi tumekuwa tukihoji kusuasua kwa safari ya mabadiliko kwenye klabu ya Simba, lakini hoja hizo zimekuwa zikipokewa kwa matusi, dhihaka, mizaha na kejeli, kitu ambacho usingekitegemea kutoka kwa watu walioamua kwa dhati kufanya mabadiliko.
Kinara wa udadisi huo alikuwa Mbunge wa Nzega (CCM), Dk. Hamisi Kigwangallah, ambaye alianzia kuhoji uteuzi wa Barbara Gonzalez kuwa ofisa mtendaji mkuu wa klabu (CEO) katika muundo mpya wa uendeshaji klabu, wakati akiwa ni mfanyakazi au mtu wa karibu wa Mohamed Dewji, ambaye anatakiwa kuwa mwekezaji wa kumiliki sehemu ya asilimia 49 za hisa za klabu walizotengewa wawekezaji.
Katika utaratibu ambao taasisi zimekubaliana kuwa na bodi ya wakurugenzi na sekretarieti, pande zote zinazohusika katika umiliki hazitakiwi ziwe na mtendaji mwenye maslahi na upande mmoja kwa kuwa ndiye anayetakiwa kusimamia maslahi ya klabu na kuwajibika kwa wanahisa. Jibu la swali la Dk. Kigwangallah likawa ni kisasi cha kunyimwa mkopo wa pikipiki na majibu hayo yakabebwa na machawa kumdhihaki waziri huyo wa zamani.
Lakini hofu yake ilikuwa ni Dhahiri. Kama CEO mwenye maslahi na moja ya pande zinazomiliki klabu anaweza kupewa maelekezo kwamba mwekezaji amekuwa akitoa fedha kwa ajili ya usajili na matumizi mengineyo ambazo zimeshafika Sh20 bilioni, nani angembishia? Ingebidi ufanyike ukaguzi kuthibitisha hilo, lakini huku kukiwa na mgogoro mkubwa.
Kama ni kweli, uamuzi wa wajumbe wa bodi ya wakurugenzi ya Simba kutoka upande wa wanachama wakiongozwa na Issa Masoud unaweza ukawa unathibitisha hofu ya Dk Kigwangallah kuhusu sekretarieti kuwa na maslahi na mwekezaji. Masoud na wenzake wamedai kuwa walipewa maombi ya mdomo kwamba bodi ipitishe azimio kwamba fedha zote ambazo Mohamed Dewji alikuwa akitoa tangu mwaka 2018 zijumlishwe na kuhesabiwa kama ndizo fedha ambazo mwekezaji ametoa kununua asilimia 49 ya hisa zilizotengwa kwa wawekezaji.
Kama ni kweli, iliwezekanaje mwekezaji kuwasiliana moja kwa moja na mhasibu ambaye yuko chini ya CEO? Na inawezekanaje ombi hilo lisipitie kwa CEO ambaye angeliwasilisha katika kikao cha bodi? Na shauri la Dk Kigwangallah linakuja pale ambako fedha hizo ni za kuanzia mwaka 2018 wakati Barbara akiwa CEO ambaye angeweza kufanya lolote kuonyesha fedha nyingi kutoka kwa mwekezaji zilitumika kuendeshea klabu maana yake kunaonekana kuwa na mawasiliano ya moja kwa moja kati ya mwekezaji na watendaji (kama maneno hayo ni kweli), kitu ambacho hakitakiwi kabisa kuwepo kwenye taasisi yenye muundo ambao bodi ndio mwajiri wa watendaji ambao mkuu wake huwajibika kwao.
Dk. Kigwangallah hakuishia hapo akafikia hadi kuhoji na kuonyesha wasiwasi kama mwekezaji alishaingiza Sh20 bilioni kama fedha za kununua asilimia 49 za hisa, lakini pia akajibiwa kwa kejeli. Baadaye ikafanyika sinema ya kukabidhi hundi mfano ya fedha hizo na kuonyeshwa hadharani. Hata hivyo, majibu kwamba fedha zimeshaingizwa ama la, hayakuwa bayana. Ilikuwa ni kama kumung’unya maneno usisikie hasa kilichosemwa ni kipi.
Lakini hayo yalikuwa yakifanyika huku Tume ya Ushindani Sawa wa Kibiashara (FCC) ikiwa imeweka kizuizi cha kuendelea kwa mchakato wa kuuza hisa na kuzipa pande mpya umiliki wa klabu. FCC ilihoji mchakato ulivyokwenda, ilihoji kufuatwa kwa sharia, ilihoji kuhusu klabu ya Simba kuporwa haki zake na kuhamishiwa kwa taasisi inayoitwa Simba Sports Club Company, ilihoji suala la kuanzishwa kwa kanuni na mamlaka husika ya soka kuhusu muundo wa umiliki ambao ungeongoza aina zote za umiliki wa klabu; za wanachama, za watu binafsi na za taasisi. Hakukuwepo na majibu sahihi na ikaonekana kama wahusika wameziba masikio na wanaendelea na wanachokijua na kukitaka.
Huku pembeni Mohamed Dewji akawa akitoa maneno kwa njia tofauti, kwa kutumia akaunti zake za mitandao ya kijamii au mahojiano na vyombo teule vya habari, akionyesha kwamba kuna watu wanamkwamisha asimiliki klabu hiyo, kuonyesha kwamba huwa anatoa fedha kwa ajili ya kununua wachezaji na katika moja ya mahojiano alisema bayana kuwa alishainunua klabu hiyo miaka mitano iliyopita.
Ni kama Dewji ndio alianzisha mchakato huo. Awali, alisema yuko tayari kuinunua Simba kwa Sh20 bilioni. Mchakato ukaanza kwa kufanya tathmini ya mali za Simba na fursa zake kibiashara. Tathmini ikaonyesha kiwango hichohicho cha Sh20 bilioni. Mchakato wa mabadiliko ya katiba ulivyoanza na kufikia hatua ya kutangaza zabuni na hatimaye Dewji kushinda zabuni ya kununua asilimia 51 za hisa, kikwazo kikawa sheria za nchi kuhusu umiliki kwamba unatakiwa uwe asilimia 51 kwa wanachama, asilimia 49 kwa wawekezaji.
Bado kiwango hicho cha fedha alichoahidi Dewji na baadaye kuthibitishwa na tathmini, ndio kikawa kiwango cha kununulia asilimia 49. Kuna kasoro hapo!
Pembeni ya sakata, mashabiki na wanachama wakawa wakipiga kelele kulaumu viongozi, hasa Murtaza Mangungu, mwenyekiti wa klabu aliyechaguliwa na wanachama, na Salim Try Again, aliyeteuliwa na Dewji kuwa mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi, ambayo haikutakiwa hata ianze kazi kwa kuwa mchakato haukuwa umeanza, achilia mbali kuwa mwenyekiti wa bodi alitakiwa ateuliwe na Murtaza Mangungu, ambaye anawakilisha upande wenye hisa nyingi.
Kutokana na kampeni hizo za mitandaoni na kwenye vyombo vya habari, wanachama na mashabiki walifikia kiwango cha kuamini kuwa mwekezaji ndiye kila kitu na alishatimiza wajibu wake wa kulipa fedha anazotakiwa kulipa na hali kadhalika kuendelea kumwaga fedha za usajili, kitu ambacho katika hali ya kawaida hakitakiwi kufanywa na mwekezaji, bali na bodi ambayo inapitisha bajeti ya matumizi kwa kila mwaka kwa imani kuwa kama hizo Sh20 bilioni zingekuwa zimeingizwa maana yake zingeimarisha mtaji wa klabu na kuiwezesha bodi kupanga bajeti kulingana na fedha hizo na nyingine ambazo klabu ilikuwa inapata kama bonasi za kushinda mataji, fedha za udhamini, fedha za haki za matangazo, fedha za huduma wakati wa mechi na mauzo ya bidhaa zake kama jezi au kukopa fedha pale inapohitaji.
Katika fedha za udhamini, mwekezaji ana bidhaa kadhaa zilizowekwa katika jezi na vipeperushi vingine vya klabu, ingawa hakujakuwepo na uwazi sana kuonyesha thamani ya udhamini kama Mo Foundation, Mo Extra na Mo 20.
Kwa hiyo mashabiki na wanachama walijiona wako sahihi kuwalaumu na hata kuwatukana viongozi kuwa wanapewa fedha za kununua wachezaji wenye ubora, lakini wanazifuja na kuleta wachezaji wabovu na hivyo wanatakiwa kujiuzulu au kutimuliwa.
Haya ni matokeo ya mchakato wa mabadiliko kutoendeshwa kwa uwazi na kulindwa na kauli za kejeli, kudhalilisha, matusi na hata kukwepesha tuhuma za ubovu na kuzihamishia kusikohusika.
Hiyo si hali inayoweza kudumu muda mrefu kwa kuwa popote kwenye watu wengi, si rahisi wote kuwa na hila. Ni lazima wawepo wenye maadili, wasiopenda kudanganya na wanaojali heshima yao mbele ya umma. Hawa watanung’unika na mambo yakizidi, hujitokeza na kusema kinachowakereketa.
Alianza Sued Nkwabi, ambaye habari zinasema alikuwa akihoji sana maendeleo ya mchakato akiwa mwenyekiti aliyechaguliwa na wanachama, lakini hakupata ushirikiano. Akaamua kujiuzulu na kwa weledi hakutaka kuitisha vikao na waandishi kuwaeleza anachopinga, bali alinyamaza na kuacha mambo yaje yalipuke yenyewe.
Hili la wajumbe wa bodi ya wakurugenzi waliochaguliwa na wanachama kujitokeza na kutoa tuhuma dhidi ya mwekezaji linaonyesha ni kiasi gani moshi unavyofukuta ndani ya uongozi wa Simba katika muundo wa sasa, ambao kitaratibu hautakiwi uwepo hadi mchakato ukamilike.
Mauzauza yamekuwa mengi katika kipindi ambacho Simba imepoteza makali yake na hakuonekani kama kulikuwa na uendeshaji timu kisayansi ulioiwezesha klabu kupata mafanikio kwa miaka minne mfululizo, kiasi cha viongozi kukaa chini na kutathmini walipokosea. Imekuwa kama wanajaribu kushika hiki na kile bila mafanikio na hali inaweza kuwa mbaya zaidi kama Simba itavuka kipindi hiki cha usajili bila ya kunyoosha mambo.
Mbali na wanachama wanaoona Mangungu na Try Again ndio tatizo, wapo wanaoona kufariki kwa Hanspope kumechangia kwa kiasi kikubwa klabu kupoteza uwezo wake katika usajili na uendeshaji timu, na wapo wanaoona kwamba kukaa kando kiasi fulani kwa wanachama wa kundi la Friends of Simba pia ni sababu ya Simba kutofanya vizuri na wapo wanaokubali kwamba Yanga imeimarika zaidi na Simba ipo palepale ndio maana upande wa pili unang’ara.
Lakini yote kwa yote, mchakato wa mabadiliko ulianzishwa ili kuondoa aina yoyote ya utegemezi kwa watu fulani binafsi, kikundi, uholela katika kufanya uamuzi na kupata mfumo bora wa uongozi na umiliki ambao hauwezi kuyumbishwa na udhaifu wa mwekezaji au watu wengine binafsi.
Lakini kufanya mabadiliko huku ukiangalia sura ndiko kumesababisha kuwepo na kasoro hizo ambazo zimeifikisha Simba ilipo leo.
Cha muhimu ni Simba kuelewa kuwa mchakato kama huo wa kubadili muundo wa uendeshaji na umiliki wa klabu ni mradi mkubwa ambao unatakiwa uzingatie misingi yote ya weledi, na hasa uwazi. Ramani ilitakiwa ichorwe ya safari ya kuelekea Simba mpya na vituo vibainishwe ili kila baada ya muda wanachama na mashabiki wataarifiwe safari imefikia wapi, mafanikio na changamoto na si kuaminishwa kuwa kila kitu kimekwenda vizuri.
Ni kama Simba imerudishwa mwanzoni kabisa mwa mchakato na hivyo, ‘akili kubwa’ ni lazima itumike kuikwamua katika mkwamo.