Tehran. Watu sita wameidhinishwa kugombea urais wa Iran katika uchaguzi utakaofanyika Juni 28, 2024. shirika la habari nchini humo la Iran International limeripoti.
Uchaguzi utafanyika kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa taifa hilo, Ebrahim Raisi aliyefariki kwenye ajali ya helikopta pamoja na wasaidizi wake huko Kaskazini Magharibi mwa Iran iliyotokea Mei 19, 2024.
Katika kufanikisha uchaguzi huo, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iran imetangaza orodha ya mwisho ya wagombea hao walioidhinishwa na Baraza la Ulinzi ambapo watachuana katika uchaguzi huo.
Orodha ya wagombea wote ina viongozi wakuu serikalini kama vile Saeed Jalili mwenye msimamo mkali ambaye ni mwakilishi wa Ali Khamenei katika Baraza Kuu la Usalama la Kitaifa, Mohammad Bagher Ghalibaf, Spika wa Bunge wa sasa na Masoud Pezeshkian, mbunge mwanamageuzi.
Wengine katika kinyang’anyiro hicho ni pamoja na mbunge wa zamani, Masoud Pezeshkian, waziri wa zamani wa sheria na mambo ya ndani, Mostafa Pourmohamadi, Meya wa Tehran, Alireza Zakani pamoja na mbunge wa zamani, Amir Hossein Ghazizadeh Hashemi.
Kuidhinishwa kwa wagombea hao na Baraza la Walinzi, chombo cha maulamaa wanaojulikana kwa utiifu kwa Kiongozi Mkuu Ali Khamenei, kutawafanya kuwa na wiki mbili za kufanya kampeni kabla ya kupiga kura.
Awali, waliojiandikisha kugombea urais walikuwa watu 80 wakiwemo wanawake wanne lakini hawakufaulu katika mchujo kama ilivyokuwa kwa chaguzi zote za urais tangu mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979.
Kuna watu kadhaa mashuhuri waliondolewa kugombea ikiwa ni pamoja na Rais wa zamani, Mahmoud Ahmadinejad, spika wa zamani wa bunge, Ali Larijani na Makamu wa Rais wa zamani, Es’haq Jahangiri.
Shirika la Habari la AFP limemnukuu Meya wa Tehran ambaye ni mmoja wa wagombea, Zakani katika chapisho lake la X akisema “atashindana hadi mwisho ili kuendeleza njia ya Raisi”.
Nchini Iran, mamlaka ya mwisho anayo kiongozi mkuu, Ayatollah Ali Khamenei (85) ambaye ameshikilia wadhifa huo kwa miaka 35 na si Rais kama ilivyo katika mataifa mengi.
Kufuatia kifo cha Raisi, Khamenei alimteua makamu wa Rais Mohammad Mokhber (68) kama Rais wa muda kwa mujibu wa Katiba ya nchi hiyo.