Dodoma. Makamu wa Rais Dk Philip Mpango amesema pale kwenye madai kuwa haki haitendeki, wahusika wafuate taratibu za kutoa taarifa kwenye vyombo vya ulinzi na usalama ili hatua stahiki zichukuliwe kwa wakati.
Dk Mpango ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Aprili 22, 2024 Jijini Dodoma kwenye maombi na dua maalumu ya kuliombea Taifa iliyofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.
Amesema pale kunapokuwa na madai ya mauaji ya raia au kuteswa wahusika wasikalie kusema tu bali wayapeleke kwenye vyombo vya ulinzi na usalama ili yafanyiwe kazi.
“Ninaomba sana tusikalie kusema tu tuyapeleke kwenye vyombo vya ulinzi na usalama na ushahidi na niwahakikishie tutayafanyia kazi kwa uadilifu,” amesema Dk Mpango.
Kuhusu ubadhirifu wa mali za umma amesema ni kweli yapo yaliyoelezwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kusema kuwa, Rais Samia Suluhu Hassan ameshatoa maelekezo kwa wizara zote zinawajibika kutoa maelezo pale palipokuwa na hoja iliyotolewa na CAG
“Hivyo, hatutasita kuchukua hatua pale ambako tumejiridhisha kuwa kuna makosa yamefanyika,” amesema.
Vilevile ameiomba mihimili yote ya dola Serikali, Bunge na Mahakama zifanye kazi kwa ushirikiano kwa maendeleo na ustawi wa nchi na watu wake na kila Mtanzania aitumikie nchi katika nafasi yake kwa haki, uadilifu na uzalendo.
Amewasihi viongozi wa dini na Watanzania kuendelea kuhubiri amani upendo na mshikamano na wasiache kukemea matendo maovu hususani ufisadi, dhuluma, ubakaji, biashara na matumizi ya madawa ya kulevya, uvunjifu wa amani na matendo yote yasiyoendana na maadili ya Kitanzania na yanayomchukiza Mungu.
Akizungumzia miaka 60 ya Muungano amesema pamoja na mafanikio makubwa yaliyofikiwa na Taifa katika kipindi hicho, bado kuna uhitaji wa kuendelea kufanya kazi kwa bidii zaidi ili kuongeza kasi ya maendeleo na kukuza ustawi wa jamii ili kutatua changamoto mbalimbali zinazolikabili Taifa.
“Katika nafasi hii napenda kusisitiza wananchi wote kuzingatia muda, bado matumizi ya muda katika Taifa letu hayaridhishi, mimi naamini katika miaka 60 mipya inayoanza baada ya siku nne tutabadilika na kutumia muda vizuri zaidi,” amesema Dk Mpango na kuongeza kuwa,
“Hali kadhalika Watanzania wote tukiongozwa na viongozi wa dini, Serikali, wazazi, walezi na walimu naomba tuwajibike kuendelea kukabiliana na mmomonyoko wa maadili katika Taifa letu unaosababisha matendo yanayokiuka mila na desturi za Kitanzania ikiwamo uhalifu, ukatili, matumizi ya dawa za kulevya na mengine ambayo hayampendezi Mwenyezi Mungu,” amesema Dk Mpango.
Pia, amewasihi Watanzania kuliombea Taifa ili Muungano udumu na uweze kuyaishi maono ya waasisi wa Taifa ya kudumisha amani, umoja na mshikamano.
Amewashukuru viongozi wa dini kwa kuendelea kukemea maovu kuonya na kufundisha maadili mema katika Taifa na kutoa huduma za kiroho na kijamii kwa Watanzania.
Amewaomba viongozi wa dini wamwombe Mwenyezi Mungu aliepushe Taifa na majanga mbalimbali yakiwamo mafuriko, kimbunga ukame matetemko ya ardhi magonjwa yaa mlipuko ambayo yanaweza kudhoofisha maendeleo ya Taifa
Amewasisitiza Watanzania kupanda na kutunza miti, kutunza vyanzo vya maji, kutunza misitu na uoto wa asili na waendelee kwa kasi zaidi kuondokana na matumizi ya nishati chafu ya kupikia na waanze kutumia gesi.
Akizungumza kwenye ibada hiyo Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda amewataka viongozi waliopewa dhamana nchini kutenda haki ili amani iweze kuwepo kwani bila kutenda haki hakuna amani itakayopatikana.
Amesema miongoni mwa maeneo yanayohatarisha amani nchini ni kwenye suala zima la kuwapata uongozi wa kitaifa, kwa kuwa kila inapofikia hatua ya kuwachagua wabunge, madiwani na Rais yanatokea maafa makubwa.
Sheikh Ponda amesema watu wanauawa wanateswa na kupoteza maisha matukio yanayofanyika na kushuhudiwa nchini.
“Mkutano wetu wa leo lengo letu ni kurekebisha hiyo hali ambayo imekuwa inaendelea huko nyuma kwa hiyo kama tunaomba dua basi tuhakikishe hii tunayoomba tunamwahidi Mwenyezi Mungu hatutafanya yale ambayo tumekuwa tunafanya huko nyuma na yakaleta maafa makubwa sana kwa wananchi,” amesema Sheikhe Ponda.
“Ikiwa dhamira yetu ni hivyo basi ile dhana ya kwamba dua yetu itapokewa inawezekana, lakini ikiwa hatuko tayari kurekebisha yale yaliyosababisha mpaka yakatokea maafa makubwa katika jamii yetu basi dua tutakuwa tumeomba lakini tusitarajie kuwa dua itapokelewa.”
Amesema wamwombe Mwenyezi Mungu aijalie nchi iendelee kuwa na amani awape busara wale ambao wamepewa dhamana ya kuongoza ili waweze kuheshimu na kufuata yale tuliyokubaliana kama Taifa na waweze kuyatekeleza kama tulivyokubaliana
“Lakini pia tutende haki katika zile nafasi au zile dhamana za uongozi, juzi hapa CAG ametoa ripoti yake, ukiangalia ripoti inaonyesha jinsi ambavyo watu wamepewa dhamana ya uongozi lakini jinsi ambayo hawatekelezi yale majukumu… ripoti inaonyesha kuna ukiukwaji mkubwa sana tena kwenye mambo muhimu kama afya, maji umeme na kadhalika kiasi kwamba huko mtaani sasa hali inakuwa ngumu sana,” amesema Sheikh Ponda.
Amesema ukienda hospitali mgonjwa anayesafisha figo anatozwa Sh250, 000 mpaka Sh300,000 na anatakiwa asafishe mara mbili kwa wiki mtu maskini anatakiwa alipe Sh600,000 kwa ajili ya kusafishwa figo hospitali.
“Lakini hii inatokana na ufisadi kwamba wananchi wanatekeleza wajibu wao wanatoa fedha na kodi lakini watu wanapewa dhamana halafu wanakiuka hiyo dhamana… katika mazingira kama haya amani haiwezi kuwepo amani inakuwepo pale watu wanapokuwa waadilifu viongozi wanatekeleza wajibu wao pale wanapokabidhiwa ule wajibu wao,” amesema.
Amesema mkutano wa leo ni mkutano muhimu wa dua kwa sababu wanakusudia kumwomba Mwenyezi Mungu jambo kubwa la amani ambalo lazima wazingatie kuwa kuna kuomba dua na kupokewa dua hivi ni vitu viwili tofauti lakini makusudio yawe ni kupokelewa dua.
“Lakini ili dua ipokelewe kuna masharti yake masharti ni kwamba ikiwa tunaomba amani yale matendo yetu yadhihirishe kwamba tunaomba amani kweli kwa hiyo kabla ya kuomba dua ni muhimu tuangalie namna tunavyoishi yale matendo yetu tunayoyafanya yatapelekea tuwe na amani au yale matendo yetu yatasababisha kuhatarisha amani iliyokuwepo.” amesema Ponda.
Amesema alipenda hayo mambo mawili yazingatiwe, kwa kuwa kuna umuhimu mkubwa wa kuangalia hali ilivyo kwenye jamii yetu huko mtaani.
Sheikh Ponda, amesema hali si nzuri katika suala la amani, “ kwa sababu katika mambo mengi tunakubaliana lakini hatutekelezi kama tulivyokubaliana na matokeo yake hiyo inasababisha kuhatarisha amani.”