DC SAME AKERWA NA KUZAGAA KWA TAKA MJI MDOGO SAME.

NA WILLIUM PAUL, SAME. 

MKUU wa wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, Kasilda Mgeni ameeleza kukerwa na uchafu unaotupwa kwenye mitaro pembezoni mwa barabara za mitaa kwenye mji huo na kumtaka mtendaji wa Mji mdogo Same kujitathimini juu ya utendaji wake.

Ameyasema hayo alipofanya ziara ya kushtukiza kukagua barabara saba za Mitaa zenye urefu wa Km 1.43 na kubaini kiwango kikubwa cha uchafu uliozagaa kwenye mitaro hiyo ikisababishwa na usimamizi mbovu kudhibiti utupati taka kihole.

“Nachukizwa sana kila nikitembelea mjini uchafu ni mwingi watu wanatupa tu takakata na hakuna hatua yeyote mnachukua, kata ya Same ndio sura ya mji msituaibishe”. alisema Kasilda.

Amewataka pia Watendaji kutimiza wajibu wao kusimamia sheria inayo ruhusu kuwatoza faini wanaohusika na kutupa uchafu akisisitiza kinyume chake watakao bainika kuzembea watachukuliwa hatua.

Aidha ameagiza miti yote iliyopandwa ambayo imeshindwa kumea ioteshwe upya kutimiza lengo la kufanya wilaya ya Same kuwa ya kijani.

Katika hatua nyingine amemtaka mkandarasi anayetekeleza ujenzi wa barabara hizo za mjini kumaliza ujenzi kufikia mwishoni mwa mwezi huu wa Juni kuwezesha wananchi kutumia barabara kwa maendeleo yao ya kiuchumi.

Alimpongeza Meneja wa TARURA Wilaya, Mhandisi James Mnene kwa kazi nzuri ya kuwasimamia wakandarasi hao kwani kazi ya ujenzi wa barabara hizo za mitaa zilizojengwa kwa kiwango cha Lami zimejengwa vizuri na kusema fedha ambayo imeletwa na Rais zaidi ya shilingi Milioni 980 imefanya kazi iliyokusudiwa ambapo mpaka sasa ujenzi wake umefikia asilimia 92 na kushukuru jitihada za serikali kuimarisha miundombinu ya barabara.


Related Posts