Tanzania kinara idadi ya nyati na simba Afrika

Arusha. Tanzania imefanikiwa kuwa kinara wa idadi kubwa ya wanyamapori aina ya nyati na simba barani Afrika.

Kwa upande wa nyati, Afrika nzima wako 401,000 na kwa Tanzania pekee, wako 225,000 ikifuatiwa na Afrika Kusini (46, 000), Msumbiji (45, 000), Kenya (42, 000) na Zambia (41, 000).

Tanzania pia inaongoza kwa kuwa na simba wengi,  kati ya 29,000 waliopo barani Afrika, Tanzania wako 17,000, ikifuatiwa na Afrika Kusini (3,284), Botswana (3,064), Kenya (2,500) na Zambia (2,500).

Hayo yamebainishwa leo Jumatatu Aprili 22, 2024 jijini Arusha kwenye hafla ya kutangaza matokeo ya sensa ya wanyamapori iliyokwenda sambamba na uzinduzi wa ripoti na taarifa ya watalii waliotembelea nchini mwaka huu.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Tawiri, Eblete Mjingo amesema matokeo hayo ni kutokana na sensa iliyofanyika katika mifumo mitatu ya Ikolojia.

Ameitaja mifumo hiyo kuwa ni pamoja na ya  Nyerere – Selous – Mikumi, Saadan – Wamimbiki na Ikolojia ya Serengeti zote zikijumuisha jumla ya kilomita za mraba 107,522.

“Sensa hii iliyotokana na mifumo mitatu ya ikolojia inalenga kutoa taarifa juu ya mwenendo wa msimu wa uwepo wa wanyama pori mashuhuri kama tembo, simba, twiga, chui na faru ambao ni vivutio vikubwa vya watalii wanaokuja nchini,” amesema Mjingo.

Waziri wa Maliasili na utalii, Angellah Kairuki akikata utepe kuzindua ripoti ya taarifa ya watalii waliotembelea nchini mwaka 2023, kushoto ni mwenyekiti  wa bodi ya Tawiri, Dk David Manyanza na Mkuu wa Wilaya ya Arusha Felician Mtahengerwa.

Amesema kwa upande wa tembo, Tanzania imejiweka kwenye nafasi ya tatu barani Afrika, kwa kuwa na tembo 60,000 wakitanguliwa na Botswana (130, 000) na Zimbabwe (100, 000).

“Nitumie nafasi hii kuitaka Serikali kuimarisha ulinzi wa wanyamapori adimu na walioko hatarini kutoweka sambamba na kuandaa mikakati ya kuwahifadhi kama sheshe na puku,” amesema.

Ametumia nafasi hiyo kuiomba Serikali kuwatengea Sh4 bilioni kwa ajili ya kufanya sensa ndani ya ikolojia zote 11 nchini, itakakayojumuisha wanyama wote bila kujali wakubwa na wadogo.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki amekubali ombi hilo na kusema tayari Rais Samia Suluhu Hassan ameshapitisha ombi hilo kwa ajili ya kufanyika kwa sensa nchi nzima.

Mbali na hilo amewataka wadau wa utalii kutumia takwimu hizo kuhakikisha wanazifanyia kazi pia waone namna ya kudhibiti shughuli za kibinadamu katika maeneo yaliyohifadhiwa.

“Serikali kwa sasa inafanya kazi ya kuongoa shoroba zilizopo nchini hivyo nisisitize matumizi ya teknolojia katika zoezi hilo kwa ajili ya  uhifadhi wanyamapori nchini na kupunguza migongano kati yao na binadamu,” amesema.

Related Posts