THRDC sasa wageukia wafadhili wa ndani

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umeanza kuhamasisha upatikanaji fedha za ndani ya nchi kusaidia shughuli za utetezi kutokana na kuwepo kwa mabadiliko katika vipaumbele vya wafadhili kutoka nje.

Inaelezwa kuwa asilimia 90 ya shughuli za utetezi wa haki za binbadamu nchini zinategemea ufadhili kutoka nje huku asilimia 10 ikitokana na kujitolea kwa wadau wa ndani na usaidizi wa makampuni.

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa, akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa Kamati ya Uhamasishaji wa Rasilimali za Ndani. Kushoto ni Mkuu wa Dawati la Wanachama THRDC, Lisa Kagaruki.

Akizungumza Juni 10,2024 na Waandishi wa habari Mratibu Taifa wa THRDC, Onesmo Olengurumwa, amesema wameunda kamati ya wakurugenzi 27 wa taasisi ambazo ni wanachama wa mtandao huo itakayohamasisha upatikanaji wa rasilimali za ndani zitakazosaidia mashirika na wadau wa haki za binadamu nchini.

“Moja ya majukumu ya msingi ya THRDC ni kuhakikisha watetezi wa haki za binadamu nchini wanakuwa na uwezo wa kifedha ili kufanya kwa ufanisi shughuli za utetezi wa haki za binadamu, mashirika mengi yamekuwa yakifanya kazi yakiwa na changamoto za upungufu wa rasilimali fedha.

“Kazi za mashirika ya utetezi wa haki za binadamu zimeleta mchango mkubwa wa maendeleo katika nchi yetu, ndiyo maana mtandao umeamua kuunda kamati ya kuweka utaratibu mzuri ili wafanyabiashara na makampuni binafsi waweze kuchangia kazi za utetezi hapa nchini,” amesema Olengurumwa.

Amesema mashirika ya haki za binadamu yanafanya kazi katika afua mbalimbali kama vile haki za wanawake, watoto, huduma za msaada wa kisheria, mabadiliko ya tabia nchi, watu wenye ulemavu, mabadiliko ya sheria, uwajibikaji, mazingira na utoaji huduma za kijamii yaani afya na nyingine.

Naye Mkuu wa Dawati la Wanachama THRDC, Lisa Kagaruki, amesema madhumuni ya jumla ya kamati hiyo ni kutoa mwongozo na kuunga mkono juhudi za mashirika ya utetezi wa haki za binadamu katika kukusanya rasilimali na kutekeleza mipango ya ubunifu ya kifedha kwa kuzingatia vyanzo vya ndani.

“Kamati imepewa jukumu la kutanua wigo wa ufadhili nchini kwa kuandaa mkakati wa kitaifa wa kushawishi sekta binafsi kusaidia mashirika yote ya haki za biadamu hapa nchini yakiwemo mashirika wanachama na yasiyo wanachama wa THRDC,” amesema Kagaruki.

Related Posts