UVCCM wataka mtandao wa X ‘ufungiwe’

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Mohamed Kawaida ameiomba Serikali kuchunguza maudhui yaliyomo katika Mtandao wa X (zamani Twitter) kwa kile alichodai kuwa yanakwenda kinyume na mila na desturi za Watanzania.

Hivi karibuni mtandao huo ulitangaza kuwa kuanzia sasa umeruhusu rasmi watu kuonyesha na kuweka maudhui ya watu wazima hatua iliyoibua mjadala mkubwa kutoka pande mbalimbali.

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Mohamed Kawaida, akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam.

Akizungumza leo Juni 11,2024 na waandishi wa habari amesema baadhi ya maudhui yanayotolewa katika mtandao huo yanaweza kusababisha mmomonyoko wa maadili nchini.

“Maudhui ya kingono na mengine si utamaduni wa Mtanzania, umefika wakati sasa kwa Serikali kuufungia mtandao huu kwa sababu hauendani na tamaduni zetu.

“Walianza kwa kutuandaa kisaikolojia wamebadilisha jina kutoka Twitter hadi X ili tuone ni neno la kawaida, watu wengi wanatumia mtandao huu hasa vijana Serikali ichukue hatua kulinda maadili ya vijana na Watanzania wote kwa ujumla,” amesema Kawaida.

Julai 2023 Mmiliki wa mtandao huo, Elon Musk, alitangaza mabadiliko ya nembo yake kutoka ndege hadi herufi X.

Related Posts