Benki ya NMB imetoa gawio la Sh. 57.4 bilioni kwa Serikali ambayo ni kiashiria cha azma ya kuleta tija na faida kubwa kwa wawekezaji wao wote, ikiwemo Serikali yenye umiliki wa asilimia 31.8 katika benki hiyo. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).
Gawio hilo lililotolewa na NMB ndilo gawio kubwa lilitolewa na taasisi za kibiashara ambazo Serikali ina hisa chache.
Akipokea hundi ya gawio hilo leo Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Samia Suluhu Hassan ameupongeza uongozi wa benki hiyo kwa kuwa mfano bora wa utendaji kutokana na mazingira bora yaliyowekwa na Serikali.
Amesema hiyo ni ishara ya matokeo mazuri ya kiutendaji yaliyopelekea kuongezeka kwa faida kwa taasisi na gawio kwa Serikali.
Hundi hiyo imekabidhiwa kwa Rais Samia na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi NMB – Dk. Edwin Mhede pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna.
Akizungumza katika hafla hiyo, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna amesema kutokana na mazingira wezeshi na uimara wa sekta ya kibenki, NMB ni miongoni mwa mabenki yaliyokua sana.
“Gawio la jumla limeongezeka kutoka Sh 97 bilioni mwaka 2021, hadi kufikia 181 bilioni mwaka 2023. Gawio kwa Serikali limeongezeka kutoka Sh 30.8 bilioni mwaka 2021 hadi kufikia Sh 57.4 bilioni mwaka 2023,” amesema na kuongeza;
“Tunawashukuru wadau wetu wote kwa kuwa sehemu ya mafanikio haya.”
Wakati wa hafla hiyo, Rais Samia pia aliikabidhi tuzo Benki ya NMB kutambua mchango wao katika kutoa gawio kubwa kwa Serikali mwaka hadi mwaka.