Dar es Salaam. Baraza la Kiswahili Tanzania (Bakita) linatarajiwa kuadhimisha juma la Kiswahili ambalo litaangazia fursa za maendeleo ya lugha hiyo duniani.
Wanazuoni na wageni kutoka nje wanatarajiwa kueleza namna wanavyojifunza Kiswahili.
Bakita limetenga siku sita kwa ajili ya maadhimisho ya siku ya Kiswahili yanayobebwa na kaulimbiu ‘Fursa za maendeleo ya kugha ya Kiswahili.’
Maadhimisho hayo yanatarajiwa kuzinduliwa Juni 29, kwa mbio za masafa marefu kabla ya shughuli mbalimbali kuanza kutekelezwa kati ya Julai 3 hadi 7, 2024 katika maeneo tofauti.
Hayo ni maadhimisho ya tatu kufanyika tangu kuanzishwa kwa siku ya Kiswahili duniani Novemba 2021.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 11, 2023 Katibu Mtendaji wa Bakita, Consolata Mushi amesema mbio hizo zitaongozwa na Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, mkoani Arusha.
Mbio hizo amesema zitahusisha kilomita mbili, tano, 10, na 21.
Amesema washindi watapewa zawadi ya fedha, medali na za utambulisho za ushiriki wao.
“Baada ya hapo maadhimisho yatahamia jijini Dar es Salaam ambako Julai 3, 2024 kuanzia saa 2.00 asubuhi katika ofisi za Bakita kutakuwa na maonyesho ya vitabu na simulizi za babu na bibi kwa ajili ya watoto,” amesema.
Julai 4, kutakuwa na mjadala wa kitaaluma ukihusisha wanazuoni watakaojadili uzoefu wa nchi za nje katika ufundishaji wa Kiswahili.
“Watu kutoka nchi za nje wataeleza jinsi wanavyojifunza Kiswahili katika nchi zao kwenye ukumbi wa maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,” amesema.
Julai 5, yatafanyika matembezi ya Kiswahili yatakayopambwa na wanafunzi wa vyuo, shule za sekondari na msingi.
“Mgeni rasmi atatumia siku hii kugawa tuzo kwa washindi wa insha za Kiswahili, washindi watatu kutoka Bara na watatu Zanzibar watapatiwa zawadi zao na shule wanazotoka,” amesema.
Amesema Julai 6 kutakuwa na mjadala utakaobebwa na mada isemayo ‘Nafasi ya mwanamke katika historia ya Afrika’ utakaowakutanisha wazungumzaji wa nje na ndani ya nchi wakielezea historia ya mwananmke alipotoka na alipo.
Julai 7 imepangwa kuwa siku ya kilele cha maadhimisho ya Kiswahili duniani ambayo yatafanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC).
“Siku hii tutatoa tuzo za kitaifa na kimataifa. Tuzo za kimataifa ni ya Mwalimu Julius Nyerere katika Kiswahili kwa kutambua mchango wake wa kukiendeleza, atakayetunukiwa tuzo hii ni Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia elimu, sayansi na utamaduni (Unesco) na itatolewa nchini Ufaransa,” amesema.