SERIKALI IMETOA BIL. 16 KWA SHULE 16 ZA WASICHANA ZA SAYANSI ZA MIKOA

Naibu Waziri Ofisi ya Rais – TAMISEMI anayeshughulikia Elimu Mhe. Zainab Katimba amesema kabla ya kukamilika kwa mwaka wa fedha 2023/24 Serikali imetoa kiasi cha shilingi Bilioni Moja kwa kila shule mpya 16 za bweni za wasichana zilizojengwa ili kukamilisha miundombinu iliyosalia.

Mhe. Katimba amesema hilo bungeni Jijini Dodoma katika kipindi cha maswali na majibu wakati akijibu la nyongeza la Mhe. Emmanuel Lekishon Shangai,Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro aliyetaka kujua ni lini Serikali itapeleka fedha kwaajili ya kujenga uzio na nyumba za watumishi katika zule hizo ambazo kwasasa ujenzi wake umefikia asilimia 85.

“Serikali imepeleka bilioni moja katika shule zote 16 za wasichana ambazo zilipelekewa bilioni tatu kwa awamu ya kwanza kwaajili ya ujenzi wa miundombinu ya msingi ikiwemo vyumba vya madarasa 10,chumba cha TEHAMA kimoja, maktaba moja, nyumba za walimu tatu na mabweni manne hivyo serikali itapeleka fedha hiyo kwaajili ya kukamilisha miundombinu ili shule zetu hizi ziweze kuwa zimekamilika na wanafunzi waweze kuingia na kuanza masomo yao” amesema Mhe. Katimba

Awali akijibu swali la Msingi la Mhe. Zaytun Seif Swai mbunge wa Viti Maalum ambaye alitaka kufahamu ni lini Serikali itaanza kujenga shule ya Wasichana Arusha ambayo ilipangwa kujengwa katika Wilaya ya Longido Kata ya Enkikret?

Mhe. Katimba amesema “Serikali kupitia Mradi wa kuboresha Elimu ya Sekondari imepanga kujenga shule 26 za bweni za wasichana za kitaifa katika mikoa yote nchini. Lengo la shule hizi ni kuongeza fursa kwa wanafunzi wa kike kusoma masomo ya sayansi na kuwaepusha na vishawishi vinavyosababisha kukatisha masomo”. Amesema

Mhe. Katimba ameongeza kuwa ujenzi wa shule hizi umefanyika katika mikoa yote kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza ilianza kwa mikoa ya Kagera, Shinyanga, Mwanza, Singida, Pwani, Songwe, Lindi, Dar es Salaam, Njombe na Ruvuma. Aidha na awamu ya pili imefanyika katika mikoa iliyobaki na kufanya mikoa yote kuwa imepokea fedha za ujenzi wa shule za bweni za wasichana za mikoa ikiwemo Mkoa wa Arusha ambapo ujenzi unafanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Longido na umefikia asilimia 85.

Related Posts