NEMC yashusha rungu miradi isiyofanya tathmini ya mazingira

Dar es Salaam. Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limetaka miradi yote ambayo haikufanyiwa tathmini za mazingira (EIA) kufanya hivyo.

Kwa yenye vyeti imetakiwa kutoa mrejesho wa tathimini wa kila mwaka kama sheria inavyotaka.

NEMC imesema hayo ikiwataka wamiliki na viongozi wa miradi ambayo haijafanyiwa EIA kufanya hivyo kwa kuwa  baraza hilo litaanza ukaguzi Agosti, 2024.

Pia, imesema itaanza ukaguzi wiki ijayo (kuanzia Juni 18) kwa miradi yenye vyeti lakini haifanyi tathmini ya kila mwaka.

Kaimu Mkurugenzi wa NEMC, Uzingatiaji na Ufuatiliaji, Hamadi Kissiwa amesema wastani wa asilimia 10 pekee ya miradi iliyowahi kupewa vyeti vya EIA ndiyo inayowasilisha tathmini za mazingira kila mwaka.

“Ni miradi michache sana inayowasilisha vyeti vya ukaguzi, hii imesababisha kuwapo migogoro baina ya wawekezaji na wananchi kwenye maeneo mbalimbali,” amesema.

Kissiwa amesema: “Unakuta mtu ana mradi wa kuyeyusha chuma chakavu ambao upo kwenye maeneo ya watu, unaleta kelele, harufu na moto lakini kumbe angefanya hivyo tungeweza shauri. Tunaweza kubaini ni mradi ulifuata watu au kinyume chake na kushauri,” amesema.

Amesema umuhimu wa kufanya uhakiki wa kila mwaka utasaidia kushauri na kufanya maboresho yatakayochangia uendelevu wa miradi na mazingira.

“Wiki ijayo tutaanza na wenye vyeti kwanza, kwa sababu kanuni za Usimamizi wa Mazingira -Tathmini ya Athari za Mazingira na Ukaguzi (Marekebisho) imeweka wazi umuhimu wa jambo hili,” amesema.

Amesema sheria inatoa adhabu kwa watakaokiuka kanuni hizo.

Kaimu Mkurugenzi, Kurugenzi ya Tathmini ya Athari ya Mazingira na Jamii Edika Masisi amesema: “Tunawataka wenye miradi ambayo haijafanyiwa thamini za mazingira ifanye hivyo mara moja kuondoa usumbufu. Baraza linatoa mpaka Agosti wenye miradi wote wafanye tathmini.”

Ametoa mfano wa miradi yenye changamoto kuwa ni wachimbaji wa madini wadogo na wa kati, akitaja sekta ya mawasiliano na nishati kama ndizo zinaongoza kwa kufanya EIA kabla ya kuanza mradi.

Amesema kutofanya tathmini kunaleta migogoro ambayo pengine ingetatuliwa kabla ya mradi kuanza.

“Wachimbaji unakuta shughuli zikianza kunakuwa na utiririshaji maji yenye sumu ambayo tatizo linaweza kuwa ni la asili kwa maana ya aina ya miamba ya pale na siyo mradi ulioleta tatizo lakini mgogoro unatokea kwa sababu hawakufanya tathmini kabla,” amesema.

Viongozi hao wamesema miongoni mwa sababu za kuwepo kwa miradi isiyo na tathmini za mazingira ni uelewa duni wa wawekezaji ambao wengi ni wageni, pia mipango miji.

Mjumbe wa bodi ya muungano wa asasi za kiraia na vyama vya wafanyakazi unaofanya uchambuzi wa sera za uwekezaji na biashara (TATIC), Stephen Msechu amesema NEMC wamechelewa kutoa maagizo hayo, akihoji inakuwaje mradi unaanza na haujafanyiwa tathmini.

“Mtu anapataje leseni ya kuanzisha mradi, tatizo ni labda NEMC wenyewe au taasisi nyingine za Serikali lakini kama wameamka ni jambo jema, inabidi wafanye hayo kwa miradi binafsi na ya umma kwa sababu unakuta shule imejengwa katikati ya makazi, au barabara inajengwa haina sehemu za kupitisha maji,” amesema Msechu.

Balozi wa Umoja wa Mataifa (UN) katika mazingira na mabadiliko ya tabianchi, Dk Aidan Msafiri ametaja mambo manne ya muhimu ya kufanya tathmini akisema:

“Ardhi tuliyonayo haiongezeki lakini watu tunaongezeka. Rasilimali zipo vilevile lazima vitu hivi viwekewe mkakati wa muda mrefu na ufanyiwe upembuzi kila baada ya muda Fulani.”

Dk Msafiri ambaye pia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Maendeleo na Mazingira (KCDE) amesema tathmini ni muhimu kwa jamii endelevu na ustawi wa jamii hiyo.

“EIA husaidia kwenye mipango miji, upangaji makazi na mazingira ya asili ya viumbehai. Kwenye miaka 100 iliyopita siyo kama sasa dunia imepoteza bioanuai kwa kiwango kikubwa,” amesema.

Related Posts