Delaware. Mtoto wa Rais wa Marekani, Hunter Biden amepatikana na hatia kwa mashitaka yote yanayohusiana na matumizi ya dawa za kulevya na umiliki wa silaha kinyume cha sheria.
Kwa makosa hayo huenda adhabu yake ikawa kifungo cha miaka 25 jela, ingawa wataalamu wanasema muda huo ni nadra sana kutokea.
Hatua hiyo inamfanya kuwa mtoto wa kwanza wa rais aliye madarakani kukutwa na hatia ya uhalifu.
Hunter Biden, mwenye umri wa miaka 54, alitikisa kichwa kidogo baada ya hukumu kusomwa lakini hakuonyesha hisia zozote.
Kisha alimgonga kwa mkono wakili wake Abbe Lowell kwenye mgongo na kumkumbatia mshiriki mwingine wa timu yake ya sheria.
Mama yake Hunter, Jill Biden alifika mahakamani dakika chache baada ya mahakama kutoa uamuzi wake.
Hunter Biden alitoka nje ya mahakama akiwa ameshikana mikono na mama na mke wake. Hawakuzungumza na waandishi wa habari, waliingia kwenye magari yao yaliyokuwa yakiwasubiri na kuondoka.
Baada ya uamuzi kutangazwa, Rais Joe Biden amesema amekubali matokeo ya kesi hiyo na “ataendelea kuheshimu mchakato wa kisheria huku Hunter akifikiria kukata rufaa,”
Biden na mkewe Jill wamesema wanajivunia Hunter, ambaye amekuwa mtulivu tangu mwaka 2019.
Licha ya kukutwa na hatia hizo, bado maswali yamebaki je, Hunter Biden atakwenda gerezani?
Hata hivyo, wataalamu wa sheria wanasema ni nadra sana angekabiliwa na kifungo cha miaka 25 kwa mashitaka matatu yakiwamo ya kukutwa na silaha.
Hata kwa shitaka la kuwa mtumiaji wa dawa za kulevya ambalo lina adhabu ya juu ya miaka 10, wachache wanaamini kuwa Biden atakabiliwa na adhabu kamili.
Akizungumza na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Profesa Dru Stevenson wa Chuo cha Sheria cha South Texas Houston alisema itakuwa ajabu na isiyokuwa ya kawaida kama Biden angepata adhabu ya karibu miaka mitano.
“Hiyo ni kwa watu ambao ni hatari sana, kama mtu ambaye tayari alikuwa kwenye orodha ya uangalizi ya FBI,” amesema.
Profesa Stevenson amesema kuna nafasi ya 50 kwa 50 ya kifungo na angeweza kutarajia kitu karibu na miezi 20.
“Ni vigumu kutabiri, lakini nadhani inawezekana sana,” amesema.
Profesa Stevenson amesema pia inawezekana kwamba Biden atapata kifungo cha nje, badala ya gerezani. Kupona kwake kutokana na matumizi ya dawa za kulevya kunaweza pia kutumiwa na timu yake ya sheria ili kupata adhabu nyepesi.
Hata hivyo, amebainisha kwamba jaji anayesimamia kesi hiyo alikataa kutoa “nafuu yoyote” kwa mawakili wa Biden wakati wa kesi.
Awali katika kesi hiyo, Jaji Maryellen Noreika alikuwa mkali kwa mawakili wa Biden wakati wa vikao vya ushahidi, alisema profesa huyo wa Texas, na mara nyingi aliwakatalia maombi ya mawakili wa utetezi.
Hiyo inaweza kuonyesha kwamba Biden anaweza kupata adhabu kali zaidi kuliko inavyotarajiwa.
Jaji Maryellen Noreika anatarajiwa kupanga kikao cha kutoa hukumu katika wiki chache zijazo. Biden pia atakutana na maofisa wa uangalizi wa wafungwa kwa ripoti ya kabla ya hukumu ambayo itatumiwa na jaji.
Kwa muda mfupi, haiwezekani kwamba atashikiliwa kizuizini. Hata katika tukio la hukumu ya kifungo, haitarajiwi kwamba Biden atalazimika kujisalimisha kwa mamlaka mara moja, badala yake, pengine atapewa tarehe ya kujisalimisha mwenyewe.
Aliyekuwa Msaidizi wa Mwanasheria Mkuu wa Marekani, Neama Rahmani aliiambia BBC kuwa baada ya hukumu, timu ya Biden itakuwa na siku 30 za kukata rufaa, jambo ambalo Rahmani alisema ni la uwezekano mkubwa.
“Hii ni kesi iliyotengenezwa kwa ajili ya rufaa,” alisema. Aliongeza kuwa kumtupa Biden gerezani itakuwa “ndoto mbaya ya kiutendaji” kwa sababu ya ulinzi anaopewa kama mtoto wa rais.
Imeandikwa na Mashirika ya habari