Tanesco Kagera kuwachukulia hatua vishoka, makandarasi wasio na leseni

Kagera. Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) mkoani hapa limejipanga kuwachukulia hatua kali makandarasi wadogo wasio na leseni na mafundi vishoka wanaovaa sare zenye nembo ya shirika hilo kuwatapeli pesa wananchi.

Vishoka hao wamekuwa wakiwatapeli wananchi  kwa ahadi ya kuwaunganisha na huduma za umeme.

Hayo yamebainishwa katika kikao kazi kilichofanyika Juni 11, 2024 baina ya Meneja wa Tanesco Mkoa wa Kagera Selemani Mgwira na makandarasi wadogo wa huduma za umeme majumbani,  ambao wana leseni kwa lengo la kupashana na kueleza changamoto wanazokutana nazo wakati wa kutekeleza majukumu yao.

Imebainika kuwa kuna baadhi ya makandarasi wadogo na mafundi vishoka wanaotumia sare za Tanesco kuwaibia pesa wananchi wakiwaahidi kuwaunganishia umeme katika vijiji vyao mkoani Kagera.

Mgwira amesema wameanza msako mkali kuwatafuta makandarasi ambao hawana leseni na vishoka wanaovaa sare zenye rangi na nembo ya shirika hilo zinazotumika kuwalaghai wananchi.

“Tumepokea taarifa za makandarasi wasio waadilifu na ambao hawana leseni pamoja na vishoka kuwaomba wananchi pesa za fomu, upimaji,  namba za malipo na hela ya kumuunganishia umeme. Tunaanza msako kuwabaini na kuwachukulia hatua,” amesema Mgwira.

Ameongeza kuwa: “Unakuta mtu amevalia sare ya watumishi wetu, ina nembo kabisa ya Tanesco, tunaomba wananchi toeni taarifa mkiwaona tukabiliane na vishoka wanaowaibia huko vijijini maana imekuwa kero, tuwabane waseme wanazitoa wapi na nani anawapa leseni,” amesema.

Edwini Gabriel, fundi umeme Wilaya ya Bukoba amekiri kuwa miongoni mwa watu wanaofanya shughuli hiyo hawana vigezo ikiwemo kutokuwa na leseni za kuwatambulisha, hivyo wanawatapeli wananchi.

“Sisi makandarasi ndio tunawapa kazi hivyo tunatakiwa kubadilika na kutowaruhusu kuingilia kazi yetu maana ndio wanawatapeli wateja wetu. Tunaomba mamlaka ziwachukulie hatua,” amesema Gabriel.

Kwa upande wake, Joseph Komba fundi umeme kutoka wilayani Karagwe amewageukia waliosimamishwa kazi Tanesco kwamba hawakukabidhi sare za kazi na wanashiriki katika kuwatapeli wananchi vijijini. “Serikali iwabaini hawa na ikishindikana majina yao yawekwe kwenye mbao za matangazo ili jamii iwatambue.

Mkazi wa kijiji Byeju kilichopo katika kata ya Mtukula, Antidius Kagina amesema aliunganishiwa umeme kwa gharama kubwa ya Sh167,000 ambapo ilimchukua miezi 12 kuunganishiwa kutokana na matapeli hao.

Alipotafutwa kuzungumzia jambo hilo, Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti Huduma za Nishati na Maji nchini (Ewura), Kanda ya Ziwa, George Mhina amesema makandarasi ambao walipewa leseni na mamlaka hiyo kwa kipindi hiki ni 1,108.

Amesema hakuna anayeruhusiwa kufanya kazi hiyo bila leseni inayomtambulisha na akibainika anakuwa amekiuka sheria na anachukuliwa hatua za kinidhamu ikiwemo kulipishwa faini ya Sh500,000 na kusimamishwa kufanya shughuli ya kufunga umeme kwenye nyumba.

“Mara nyingi makandarasi wa aina hiyo ndio wanaosababisha nyumba za watu kukumbwa na majanga ya moto, hivyo Ewura haturuhusu mafundi vishoka kufanya shughuli hiyo wala mkandarasi yoyote ambaye hana sifa, tunaomba wananchi mtoe taarifa mkiwabaini,” amesema Mhina.

Related Posts