Kulingana na maafisa wa utawala wa Kyiv, makombora yalivurumishwa kutoka kusini mara kadhaa, pamoja na ndege hizo zisizo na rubani zikiulenga mji mkuu.
Mashuhuda wamesema walisikia angalau mripuko mkubwa katika mji mkuu, ambapo tahadhari ya uvamizi wa anga ilidumu kwa saa mbili. Kwa mujibu wa polisi, shambulizi hilo lilisabisha moto na kumjeruhi mtu mmoja.
Soma pia: Zelensky ahimiza Ukraine isigawanywe na Urusi
Mashambulizi ya mara kwa mara katika miundo mbinu ya nishati, yamesababisha uhaba mkubwa wa umeme.
Wizara ya nishati ya Ukraine imesema inakusudia kuagiza kiasi kikubwa zaidi cha nishati ya umeme kutoka Ulaya ili kukidhi mahitaji ya raia wake.
Tangu kuanza kwa vita dhidi ya Urusi, Ukraine imeimarisha ulinzi wa anga kwenye mji mkuu, ambako mashambulizi kwa kawaida hufanya uharibifu mdogo.
Mashambulizi ya mara kwa mara ya Urusi kote Ukraine yanapunguza ulinzi wa anga wa nchi hiyo, na yamemfanya Rais Volodymyr Zelensky kuomba msaada kutoka kwa washirika.
Hivi karibuni, Zelensky ametoa wito wa msaada zaidi wa mifumo ya ziada ya ulinzi wa anga ya Patriot, kulilinda eneo la mashariki la Kharkiv linalopakana na Urusi.
Vyombo vya habari vya Marekani vimeripoti kuwa nchi hiyo itatuma mfumo huo wa ulinzi wa anga kwa Ukraine katika siku zijazo.
Urusi yafanya luteka za kijeshi
Urusi imesema kwamba jeshi lake la baharini la wilaya ya kaskazini ya Leningrad inayopakana na wanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Norway, Finland, Poland, Estonia, Latvia na Lithuania zilishiriki katika mazoezi ya mbinu ya silaha za nyuklia.
Soma pia:Belarus yasema inaungana na Urusi kwenye luteka za pili za kijeshi
Hatua hiyo inaonekana kuongeza eneo la kijiografia kwa mazoezi ya nyuklia yanayojumuisha askari kutoka wilaya za kijeshi ambazo zipo karibu na maeneo yote ya mpaka wa Urusi na Ulaya, kutoka Bahari ya Aktiki hadi Bahari Nyeusi.
Mwezi uliopita, Rais Vladimir Putin aliamuru mazoezi kama hayo kufanyika katika wilaya inayopakana na Ukraine, baada ya kile alichodai kuwa ni ishara kutoka kwa maafisa wa Magharibi kwamba wangeiruhusu Ukraine kushambulia zaidi ndani ya Urusi kwa kutumia silaha za Magharibi.