Wabunge waibana Serikali madeni ya bilioni 285 kwa watumishi

WABUNGE wameita Serikali kuanza kulipa riba ya madeni watumishi wa umma yanayohusu likizo, uhamisho, na kusafirisha mizigo baada ya kustaafu kama inavyofanya kwa wakandarasi ambao wanacheleweshewa malipo yao. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Pia wameitaka Serikali kuzingatia muongozo wa 2009 wa kanuni za utumishi wa umma unaohusu udhibiti wa ongezeko la madeni ya serikali kwa watumishi wa umma kwa sababu licha ya kutoa muda wa miezi 12 kwa madeni hayo kuliwa, bado utaratibu huo umeendelea kuwekwa kando.

Issa Mtemvu

Hayo yameibuliwa leo Jumatano bungeni jijini Dodoma na Mbunge wa Kibamba, Issa Mtemvu (CCM) aliyehoji ni lini serikali italipa madeni hayo lakini pia ni lini itapeleka bungeni muswada wa sheria ili madeni yanayocheleweshwa nje ya muda yalipwe pamoja na riba.

Naye Mbunge wa Viti Maalimu, Ritha Kabati alihoji ni muda gani unaopaswa kuzingatiwa kulipwa kwa madeni hayo kwa sababu wapo wastaafu wameshindwa kusafirisha mizigo yao.

Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Ridhiwan Kikwete amesema hadi kufikia tarehe 30 Aprili 2024 madeni ya watumishi wa umma yaliyohakikiwa na kukidhi vigezo vya kulipwa yanayohusu likizo, uhamisho na kusafirisha mizigo baada ya kustaafu ni jumla ya Sh 285.1 bilioni.

“Katika kipindi cha Julai, 2023 hadi Aprili, 2024 madeni ya jumla ya Sh 55.9 bilioni yamelipwa. Aidha, Serikali itaendelea kulipa madeni ya watumishi yasiyo ya kimshahara kila mwaka kwa kuzingatia taarifa ya uhakiki wa madeni,” amesema.

Kuhusu ni lini serikali italipa madeni hayo na lini itapeleka muswada wa sheria kuruhusu watumishi wanaodai madeni hayo kulipwa pamoja na riba, Kikwete alikwepa kujibu na kuendelea kusisitia waajiri wazingatie kanuni za muongozo huo.

Hata hivyo, Waziri mwenye dhamana, George Simbachawene naye aliongeza kuwa mamlaka za serikali za mitaa ndizo zinazozalisha madeni mengi ya upande wa uhamisho na kusafirisha mizigo baada ya kustaafu hivyo wabunge wanapaswa kufuatilia kwenye kamati za fedha za halmashauri kuhakikisha madeni hayo yanalipwa.

Alisema serikali inahusika kwenye upande wa madeni ya mishahara ya watumishi ambayo imeendelea kulipa na sasa zaidi ya Sh 169 bilioni zimelipwa.

Related Posts