Dodoma. Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile amesema Serikali za Tanzania, Zambia na China ziko katika hatua za mwisho za mazungumzo ya kuifumua reli ya Tanzania na Zambia (Tazara) kwa lengo la kuiboresha.
Kihenzile amesema jana Juni 11, 2024 bungeni wakati wa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Mlimba, (CCM), Godwin Kunambi, aliyehoji ni nini mkakati wa Serikali kuboresha reli hiyo, kuongeza mabehewa na safari za reli ya Tazara kutoka Dar es Salaam kwenda Mbeya ambayo ni tegemeo la wananchi wa jimbo lake.
Akijibu swali hilo, Kihenzile amesema reli hiyo ilijengwa mwaka 1975 baina ya Serikali tatu ambazo ni China, Tanzania na Zambia.
Amesema katika kipindi chote ilisanifiwa kujengwa kwa uwezo wa kubeba metric tani milioni tano, lakini kutokana na ubovu wa miundombinu haikufikia lengo hilo.
Kihenzile amesema habari njema ni kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amefanya kikao na Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema pamoja na Rais wa China, Xi Jinping kuhusiana na reli hiyo.
“Hivi ninavyozungumza tuko katika hatua za mwisho za majadiliano, reli nzima inakwenda kufumuliwa upya, moja kuongeza uwezo wa reli wa kubeba mizigo pamoja na kuongeza vichwa na mabehewa ya kutosha ya mizigo na abiria.
“Kwa hiyo, wakazi wa Mlimba na watumiaji wa reli hii inayotoka Dar es Salaam mpaka Kapiri Mposhi nchini Zambia (umbali wa kilomita 1,860) waendelee kusubiri habari hiyo njema inayokuja kwa Watanzania wote,” amesema.
Naye Mbunge wa Viti Maalumu, (CCM), Neema Mgaya amehoji mkakati wa Serikali wa kuwa na mabehewa yenye ubaridi katika reli ya Tazara, ili wananchi waweze kusafirisha parachichi, mbogamboga kwa kuwa zitasaidia bidhaa hizo ziwafikie walaji zikiwa na ubora.
Akijibu swali hilo, Kihenzile amesema watakapokwenda hatua ya pili ya maboresho ya reli hiyo watazingatia uwekezaji wa mebehewa yenye ubaridi.
Kwa upande wake, Mbunge wa Mlalo (CCM), Rashid Shangazi amesema Serikali imeboresha Bandari ya Tanga, hatua inayoanya kuongezeka kwa shehena ya mizigo na reli iliyopo ni chakavu.
Shangazi amehoji nini mpango wa Serikali wa kuboresha reli ya kutoka Tanga kwenda Dar es Salaam na kutoka Tanga kwenda Arusha, ili kuondoa shehena kwa urahisi.
Akijibu swali hilo, Kihenzile amesema mwaka 2023/24, Serikali ilisaini mkataba wa kununua malighafi na kwa mwaka 2024/25, Serikali inaanza kuifumua reli kati ya Tanga na Arusha yeye urefu wa kilomita 533 na kujenga reli yenye uwezo mkubwa na itakuwa inatumia takribani saa nne.
Katika swali la msingi Mbunge wa Namtumbo (CCM), Vita Kawawa, amehoji mpango wa ujenzi wa reli ya Kusini umefikia wapi.
Akijibu swali hilo, Kuhenzile amesema Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC) imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Mtwara hadi Mbambabay na matawi yake ya Liganga na Mchuchuma yenye jumla ya kilomita 1,000.
Amesema mradi huo ni miongoni mwa inayopendekezwa kupatiwa ufadhili wa fedha za maandalizi kupitia mfuko wa miradi wa nchi za ukanda wa Kusini mwa Afrika.
Amesema kwa sasa timu kutoka Benki ya Afrika Kusini, ilikuja Tanzania kwa ajili ya kufanya uthibitisho wa nyaraka za mradi ili kuendelea na hatua nyingine za upatikanaji wa ufadhili wa fedha zitakazotumika kumlipa mshauri elekezi.
Kihenzile amesema mshauri huyo atakuwa na jukumu la kupitia andiko, kuandaa makabrasha ya zabuni kwa ajili ya kumpata mwekezaji kwa utaratibu wa ubia baina ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP).