ACT Wazalendo wapinga TAMISEMI kusimamia uchaguzi serikali za mitaa

Chama cha ACT Wazalendo kwa kushirikiana na Asasi za Kiraia kinatarajia kufungua kesi kuzuia hatua za maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa zinazoendelea kuchukuliwa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).  Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Pia kimesema kitaenda kwenye kikao cha wadau kilichoitishwa tarehe 15 Juni 2024 Dodoma kuieleza TAMISEMI isimamishe mara moja mchakato inaoendelea nao wa maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa sababu ni batili na unavunja sheria za nchi.

Mohamed Mchengerwa


Hayo yamebainishwa leo Jumatano na Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu kupokea barua kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Siasa kuwajulisha kuwa TAMISEMI) inaendelea na maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kwamba 15 Juni 2024 itafanya kikao cha wadau kukusanya maoni ya rasimu ya kanuni zitakazosimamia uchaguzi huo.

Ado amesema ACT Wazalendo imesikitishwa na hatua hiyo ya TAMISEMI kwa sababu ni kinyume na Sheria na inavunja kabisa misingi ya falsafa ya 4R ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa sababu zifuatazo:

Amesema kwa mujibu wa kifungu cha 10(1)(c) cha Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi ya Mwaka 2024, Tume Huru ya Uchaguzi imepewa jukumu la kusimamia uchaguzi wa mitaa, vijiji na vitongoji.

Amesema msimamo wa muda mrefu wa chama hicho ni kuwa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa usimamiwe na Tume Huru ya Uchaguzi badala ya TAMISEMI.

“Ndiyo maana ACT Wazalendo tulishiriki kikamilifu kuhakikisha kuwa Bunge linapitisha kifungu cha Sheria kuwezesha jambo hilo. Ni jambo la kusikitisha kuwa Serikali hadi leo inasuasua kupeleka muswada Bungeni kutekeleza matakwa haya ya Sheria na badala yake inataka kuvunja Sheria kwa kuipa madaraka TAMISEMI kusimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa,” amesema.

Amesema sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Namba 1 ya Mwaka 2024 imefuta kwa pamoja (consequencial amendment) Sheria ya Taifa ya Uchaguzi ya Mwaka 1985 na Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa ya Mwaka 1979.

Amesema hatua yoyote inayochukuliwa na TAMISEMI hivi sasa kuhusiana na usimamizi wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni batili na ni kinyume na sheria.

Amesema pamoja na mambo mengine, msimamo ww chama hicho ni kufuatia hali inayoendelea na kutokana na unyeti wa jambo lenyewe, chama hicho kitaandaa kikao maalum na kuvialika vyama vingine vya siasa kuweka msimamo wa pamoja juu ya kuizuia TAMISEMI kusimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Pia kitaweka msimamo wa kuteuliwa wajumbe wapya wa Tume Huru ya Uchaguzi ili wachukue nafasi ya waliopo sasa kwa mujibu wa sheria, ambao ndio waliovuruga uchaguzi wa 2020.

“ACT Wazalendo tunasisitiza kwamba hatua hii ya TAMISEMI kupora madaraka ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kinyume na sheria za uchaguzi inatia doa kubwa falsafa ya 4R ya Rais Samia Suluhu na inapaswa kupingwa na wadau wote wa demokrasia nchini Tanzania,” amesema.

Related Posts