MFUKO WA UWEKEZAJI WA PAMOJA (TIMIZA FUND) WAZINDULIWA ZANZIBAR

Na Fauzia Mussa- Maelezo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Dkt. Saada Mkuya Salum amesema Mfuko wa uwekezaji wa pamoja TIMIZA FUND utaisaidia Serikali kuhakikisha inawashirikisha Wananchi wake katika uwekezaji na shughuli za kiuchumi kwa lengo la kuboresha kipato cha kuendesha Maisha yao.

Katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake huko katika Ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege, na Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Juma Makungu Juma wakati wa uzinduzi wa Mfuko huo amesema Mfuko huo utatoa fursa kwa Wananchi wa kipato cha chini kushiriki katika uchumi na kuongeza kiwango cha utumiaji wafedha na uchumi jumuishi.

Hata hivyo dkt.Saada ameutaka Uongozi wa Mfuko wa Uwekezaji wa pamoja TIMIZA FUND na Wadau kuyafanyia kazi mambo yote walioyaahidi katika Waraka wa toleo la Mfuko huo ili kuendelea kujenga imani kwa wananachi.

“Usimamizi wenye weledi na uadilifu wa TIMIZA FUND unategemewa katika kuleta maendeleo makubwa zaidi hivyo sote tunaojihusisha na sekta hii, twendeni tukayafanye tunayoyasema kwa mujibu wa Sheria na Kanunui zinazotuongoza”amesema Dkt.Saada.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Zan Securties Bw. Raphael Masumbuko amesema mfuko wa uwekezaji wa pamoja utasaidia kufungua milango ya fursa mbalimbali hata zile zilizopo nje ya uwezo wa mtu mmoja mmoja kwani uwekezaji huo ni kwa Watu wote wa vipato vya aina zote.

Mapema Mwenyekiti wa Bodi ya Zan Security Abdisalaam Issa Khatib amesema Mfuko huo ni chachu ya kuleta mabadiliko ya tamaduni na hamasa za wawekezaji kuweka akiba ili kuleta ushindani wa Mifuko na kuleta tija kwa Mifuko na Taifa kwa ujumla.

Amesema jambo hilo ni la kihistoria katika sekta ya uwekezaji kutokana na umuhimu wa Masoko na Mitaji ya Zanzibar.

Hata hivyo ameiomba Serikali kushauri taasisi za umma kuwekeza katika sekta ya mitaji na kujiorodhesha katika Soko la hisa ili kutoa hamasa kwa Mifuko ya uwekezaji.

Akizungumza kwa niaba ya Mtendaji Mkuu Soko la hisa la Dar-es-Salaam Bw. Emanuel Nyalali ameishukuru Serikali kwa kuanzisha sera na kanuni zinazowezesha sekta za Masoko na Mitaji kukuwa Nchini.

Ametoa wito kwa wafanyakazi kuwekeza katika Mfuko huo ili kutimiza malengo waliojipangia ikiwemo kuwekeza kwa ajili ya mahitaji ya elimu, ujenzi,ukarabati wa nyumba, kustaafu,, Gharama za safari za likizo, pamoja na huduma za afya.

Mfuko wa uwekezaji wa pamoja umeanzishwa mwaka 2019 chini ya Zan Securties Kwa Lengo la kuwashirikisha wananchi kujiunga na Mfumo wa Masoko ya mitaji na dhamana ili kunufaika kiuchumi.
Naibu Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Fedha na Mipango Juma Makungu Juma wakati akizindua mfuko wa uwekezaji wa pamoja (Timiza Fund) huko golden Tulip uwanja wa Ndege Zanzibar

Related Posts