Gairo. Wakazi wa Kijiji cha Ngiloli kilichopo katika Wilaya ya Gairo mkoani Morogoro wameiomba Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) wilayani humo kuwafikishia huduma za maji kwenye ili kuondokana na adha wanayoipata.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Juni 12, 2024, mkazi wa kijiji cha Ngiloli, Mariam Elias amesema ukosefu wa huduma ya maji safi na salama kwenye eneo wanaloishi linaleta usumbufu kwa wanawake.
“Tunaamka usiku kwenda kutafuta maji tena ya madimbwi na ya kwenye visima kwa kupanga foleni na unaweza kuamka muda huo ukaishia kupata ndoo mbili mpaka tano ambazo hazikidhi mahitaji,” amesema.
Kwa upande wake, Yusuph Mkunda mkazi wa kijiji hicho, amesema ukosefu wa maji safi na salama unasababisha wanawake kuamka usiku wa manane kufuata maji, jambo ambalo ni hatari.
“Kutokana na tatizo la maji kwenye kijiji chetu, wanawake wanahangaika kupata maji salama maana yaliyopo kwa sasa yanatoka kwa mgao ambapo tunakaa siku tatu hadi tano bila kutoka kipindi hicho wanawake ndio wanaohangaika. Tunaomba maji yasogezwe kwa wananchi na yapatikane wakati wote,” amesema.
Mkunda amesema maji yanapokosekana kwenye chanzo kilichochimbwa na Serikali, wananchi wanateka maji kwenye madimbwi na mabondeni ambayo siyo salama kwa matumizi ya binadamu, hivyo ameiomba Serikali kuongeza upatikanaji wa maji.
Akilizungumzia hilo, Meneja wa Ruwasa Gairo, Gilbert Isaack amekiri kuwepo kwa changamoto ya upatikanaji wa maji wilayani humo.
“Ni kweli tuna changamoto ya maji na awali tuliahidiwa na Serikali kuu kuletewa mabomba ya kusambaza maji na tunavyozungumza tumeshapokea yenye gharama ya Sh700 milioni na tutaanza kutandaza ili maji yawafikie wananchi kwenye maeneo yetu.”