Dodoma. Serikali imesema hadi kufikia Aprili 30, 2024, madeni ya watumishi wa umma yaliyohakikiwa na kukidhi vigezo vya kulipwa yanayohusu likizo, uhamisho na kusafirisha mizigo baada ya kustaafu ni Sh285.17 bilioni.
Hayo yamesemwa leo Jumatano Juni 12 2024 na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais -Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete wakati akijibu swali la mbunge wa Kibamba (CCM), Issa Mtemvu aliyehoji hadi sasa Serikali ina madeni kiasi gani ya watumishi wa umma yanayohusu likizo, uhamisho, na kusafirisha mizigo baada ya kustaafu.
Akijibu swali hilo, Ridhiwani amesema hadi kufikia Aprili 30, 2024 madeni ya watumishi wa umma yaliyohakikiwa na kukidhi vigezo vya kulipwa yanayohusu likizo, uhamisho na kusafirisha mizigo baada ya kustaafu ni Sh285.17 bilioni.
Ridhiwani amesema Julai 2023 hadi Aprili 2024 madeni ya jumla ya Sh55.94 bilioni yalilipwa.
Amesema Serikali itaendelea kulipa madeni ya watumishi yasiyo ya kimshahara kila mwaka kwa kuzingatia taarifa ya uhakiki wa madeni.
Katika swali la nyongeza, Mtemvu amesema Serikali inasimamiwa na Kanuni za Utumishi wa Umma za Mwaka 2009 zinazotaka madeni ya watumishi wa umma yalipwe ndani ya miezi 12.
“Sasa ni lini Serikali itasimamia mwongozo huu wa kikanuni,” amehoji Mtemvu.
Pia, amesema madai mengine ya wazabuni na makandarasi yanapochelewa kulipwa hulipwa na riba.
Amehoji Serikali haioni umuhimu wa kupeleka sera na sheria bungeni ili iweze kuwa nafasi ya kulipa riba kwa watumishi wa umma wanaocheleweshewa stahiki zao ili haja ya kuwalipa iende kwa kasi.
Akijibu maswali hayo, Ridhiwani amesema Mwongozo wa Mwaka 2009 anaouzungumza mbunge huyo, unahusu udhibiti wa madeni ya Serikali kwa watumishi wa umma.
“Ni kweli kama anavyosema mheshimiwa mbunge Serikali ilieleza pamoja na mazingatio mengi yaliyoelezwa ndani ya mwongozo huo lakini moja ya jambo la msingi kabisa ni kuhakikisha Serikali inakuwa na mpango mzuri kwa ajili ya kuridhisha madaraka,” amesema.
Amesema mara nyingi mwongozo huo unafanywa kwa kupitia bajeti zao na kumhakikishia mbunge huyo kuwa Serikali inaendelea kusimamia mwongozo huo.
Ridhiwani amesema pale panapotokea upungufu Serikali kupitia Katibu Mkuu wa ofisi yake, huwa inapeleka maelekezo na kuendelea kukumbusha maofisa waajiri juu ya kuendelea kusimamia mwongozo huu.
Kuhusu riba, Ridhiwani amemtoa hofu mbunge na Bunge kuwa Serikali inaendelea kusimamia jambo hilo kwa kuhakikisha madeni yote yaliyohakikiwa na taarifa zake zimepelekwa kwenye mamlaka husika kwa ajili ya malipo, yanalipwa.
Mbunge wa viti maalumu, (CCM), Rita Kabati amesema changamoto hiyo ya madeni ya watumishi wa umma ilijitokeza katika wilaya zote za Mkoa wa Iringa pindi waziri (hakumtaja) alipofanya ziara.
“Wafanyakazi wanapata shida sana, wanashindwa hata kutafuta nyumba nyingine za kuhamia na wengine wameshindwa kusafirisha mizigo yao kule ambako wanatakiwa waende baada ya kustaafu,” amesema Kabati.
Amehoji ni kipindi gani mtumishi anatakiwa kudai madai hayo kwa sababu yanachukua muda mrefu kiasi ambacho wanapata mateso makubwa sana.
Akijibu swali hilo, Ridhiwani amesema mwongozo wa mwaka 2009, unaelekeza nini kifanyike kabla ya kupandisha watu madaraja, hawajastaafu na kuwa ni vyema mwongozo huu ukafuatwa kwa uko wazi kabisa.
“Mwongozo unaelekeza nini kifanyike kabla ya kufika huko katika madeni lakini nataka kumhakikishia mheshimiwa mbunge madeni haya yanatakiwa yadaiwe muda wowote ambao mtu anatakiwa kulipwa stahiki zake kwa mujibu wa mwongozo uliotolewa,” amesema.
Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amesema maadeni ya watumishi yamegawanyika katika aina mbili.
Amesema yako yanayotokana na suala la mishahara ambayo wahusika ni wizara yake lakini madeni yanayotokana na mambo yasiyo ya mshahara ikiwamo uhamisho, kusafirisha watumishi baada ya kustaafu na likizo mhusika ni mwajiri au sekta husika.
“Sasa mwajiri anayezalisha madeni mengi ya namna hii Serikali za mitaa ambako sisi waheshimiwa wabunge tuko kwenye mamlaka zile. Nimesimama kuomba ombi moja, ajenda zinapozungumzwa kwenye kamati ya uongozi na fedha, moja ya vitu ambavyo waheshimiwa wabunge tuwe tunahoji ni je madeni haya yanayohusika mizigo, masuala ya likizo, uhamisho ni kiasi gani yanadaiwa,” amesema.
Amesema hiyo inatokana na madeni hayo kuzalishwa kwenye Serikali za mitaa.
“Sisi wenyewe tukishughulika kule tutapunguza mzigo. Tangu Serikali ya awamu ya sita imeingia madarakani imejitahidi sana kulipa madeni tumelipa Sh167.98 bilioni lakini bado mzigo unaendelea kuongezeka,”amesema.
Amesema kwenye Serikali za mitaa kunazalisha madeni kwa kuwa bado kunatokea uzembe wakati kila mwajiri anatenga bajeti katika kushughulikia uhamisho, likizo na mambo mengine.
Amesema wakienda kusimamia huko wanaweza kusaidia watumishi wakawa hawadai lakini pia Serikali ikawa haidai.