Bukoba. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeeleza kukerwa na kauli ya baadhi ya viongozi wa Serikali na chama kilichopo madarakani kuwa kila fedha zinazotolewa kwa ajili ya maendeleo nchini, ni za Rais Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Bukoba mjini mkoani Kagera leo Aprili 22, 2024 baada ya maandamano, Mbowe amesema kutokana na watendaji serikalini kudai kila fedha ni ya Rais Samia badala ya Serikali, nchi inaonekana ya ovyo.
“Nchi hii ni ya ovyo…yaani kila fedha inayotolewa ni ya Mama Samia hadi tunajiuliza huyu mama Samia ana kiwanda cha noti?
Mama katujengea shule, mama ameleta zahanati, mama amewajengea hospitali, mama amejenga barabara, mama ameshusha fedha..mama mama..mimi nimekaa kikao na Mama Samia nikamwambia kama kuna kitu kitakugharimu ni dhambi ya kukubali sifa ambazo hustahili. Unajua fedha sio za kwako ni kodi ya wananchi, unaambiwa mama ameshusha fedha unajua ni upande wa uchawa nawe unakaa kimya,” amedai Mbowe.
Amesema huu si wakati wa kuzungumzia fedha za miradi zinatolewa na nani, kwa sababu inajulikana zinakotoka.
“Tunataka Serikali isikilize hayo tunayolalamikia na iyatekeleze badala ya kuyapa kisogo,” amesema.
Amesema mpaka sasa Serikali haijataka kusikiliza ujumbe wao walioutoa kwenye maandamano yaliyofanyika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza na Mbeya ukiwamo wa kupanda kwa gharama za maisha na Katiba mpya.
“Tulidai gharama za maisha ya wananchi zimepanda, hawa wenzetu wanaotunga sheria za kodi, sheria za tozo na sheria nyingine mbalimbali zinazoumiza wananchi hawana uchungu hawajui wananchi wa kawaida wana mateso ya kiasi gani,” amesema Mbowe.
Amesema walipendekeza pia namna ya kupunguza ukali wa maisha kwa wananchi, akidai unatokana na gharama kubwa za kodi ambazo hazifanani na kipato cha Watanzania.
“Tukataka Serikali ipeleke bungeni muswada wa namna ya kupunguza gharama za mafuta, gharama kwenye bidhaa muhimu kama sukari na pembejeo za kilimo ili mwananchi wa kawaida aone neema ya kuzaliwa Tanzania, hawakutusikia na tukaomba yafanyike marekebisho ya msingi kwenye sheria za uchaguzi, pia hawakutaka,” amesema mwenyekiti huyo.
Mbowe amedai kupitia maandamano yaliyopita, Chadema kilitaka Serikali ijifunze kusikiliza maoni ya Watanzania, lakini bado inafanya uamuzi bila kujali maoni ya wananchi.
Hata hivyo, aliwageukia pia viongozi wa chama hicho kuwa wasiyachukulie maandamano hayo kama mzaha.
Amesema yanaonyesha hisia za wananchi… “Sio kila chama kinaweza kuandamana kwa kuwa havina ushawishi kwa wananchi wa kawaida kama kilivyo Chadema.”
Hivyo, amewataka viongozi wote wa Chadema kutambua kuwa maandamano hayo ni turufu yao kuelekea chaguzi zijazo.
Katika hatua nyingine, Mbowe amewataka viongozi wa Chadema kuweka mkakati wa kuhakikisha wanapata majimbo sita ya ubunge kati ya tisa yaliyoko mkoani Kagera.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), John Pambalu amesema wanataka kusikia kauli ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Camillus Wambura juu kauli ya ‘tutawapoteza’ hatua gani zimechukuliwa dhidi ya Mwenyekiti wa UVCCM Mkoani Kagera, Faris Buruhan.
“Tunataka kusikia jeshi limefanya nini ndani ya siku saba, Buruhan aseme kina Azory Gwanda wako wapi? Aseme kina Beni Saanane wapo wapi na kama watashindwa tutawasaidia, nia ya kuwasaidia tunayo, nguvu ya tunayo tutawasaidia,” amesema Pambalu.