MWANZONI mwa mwezi huu tuliripoti, ishu ya Kocha Mkuu wa Yanga Princess, Mzambia Charles Haalubono anatarajiwa kutimka kikosini hapo na kumpisha Edna Lema ‘Mourinho’.
Sasa habari za uhakika ni kwamba baada ya mazungumzo ya muda mrefu hatimaye Mourinho amekubaliana na viongozi wa timu hiyo kuinoa kwa msimu ujao.
Mmoja wa viongozi wa Yanga (jina tunalo) aliliambia Mwanaspoti kuwa, Edna tayari amesaini mkataba wa mwaka mmoja.
“Tunasubiri Kocha Charles amalizie kusimamia michezo miwili iliyosalia kisha tutamtangaza Edna kuwa kocha mkuu alitoa masharti ya kutaka majukumu ya kuingia sokoni mwenyewe kusajili ili kupata wachezaji wenye ushindani,” alisema kiongozi huyo.
Tulipomtafuta mwenyewe juu ya usajili huo aliendelea kusisitiza kuwa “Ni kweli sina mkataba na Biashara lakini tusubiri kama ni kweli mtajua tu.”
Edna sio mgeni katika kikosi hicho kwani kabla ya kwenda Biashara United ya Mara iliyopo Chamspionship aliwahi kupita Yanga Princess.