MASHINDANO ya 48 ya kandanda ya Kombe la Amerika ya Kusini, Copa America, yatakayofanyika Marekani kuanzia Juni 20 hadi Julai 24 yanasubiriwa kwa mengi, mbali ya kujua nani atalibeba kombe hili litakaloshindaniwa na mataifa 16.
Lakini moja lililozusha shauku kubwa ni je, mchezaji maarufu wa Argentina, Lionel Messi, ambaye sasa ana miaka 36 atastaafu kulichezea taifa hilo kama alivyoahidi au atasubiri kushiki fainali za Kombe la Dunia zitazofanyika Mexico, Canada na Marekani.
Kustaafu kwake kumetanguliwa na tangazo la Shirikisho la Kandanda la Argentina lilioeleza mara baada ya kustaafu itakuwa marufuku kwa mchezaji yeyote wa Argentina kuvaa sare namba 10 ambayo Messi anavaa.
Uamuzi huu umezusha mjadala mkubwa Argentina ambako namba 10 katika kandanda inapendwa sana na ni kawaida kusikia wachezaji wa timu za vijana wakipigana kwa kila mmoja kutaka yeye avae jezi iliyoandikwa namba 10 mgongoni.
Mapenzi ya jezi namba 10 kwa mashabiki wa kandanda wa Argentina yalianza hata kabla a Messi kuzaliwa nah ii imetokana kwa Argentina kutoa wachezaji wengi mahiri waliovaa namba hio mgongoni kwa zaidi ya nusu karne hivi sasa.
Hii imesababisha baadhi ya mashabiki na waandishi wabobezi wa michezo wa Argentina kueleza kwamba kuzuia namba hio isitumike kwa ajili ya kuheshimu mchango wa Messi pekee sio sahihi.
Wanachotaka ni iwe kuheshimu wachezaji wote mahiri wa Aregentina waliovaa sare iliyoandikwa namba 10 mgongoni na sio Messi peke yake.
Hii inatokana na kuwepo wachezaji 14 katika nusu karne iliyopita waliovaa jezi namba 10 ambao waliisaidia Argentina kubeba makombe mengi ya kimataifa, ikiwa pamoja na Kombe la Copa America na Kombe la Dunia.
Orodha ya wacheaji hawa ni pamoja na Diego Maradona ambaye alikuwa mchezaji namba moja duniani katika miaka ya 1980 na kuiongoza nchi hio kubeba Kombe la Dunia 1986 na kuwa mchezaji bora na mfungaji wa magoli mengi.
Mwingine aliyevaa jezi namba 10 ya Argentina ni Mario Kempes aliyekuwa nyota wa ushindi wa nchi hiyo wa Kombe la Dunia katika mwaka 1978 ambapo pia alitangazwa Mchezaji Bora wa mwaka huo wa Amerika ya Kusini.
Kiungo mshambuliaji, Ariel Arnaldo Ortega, naye anaingia katika orodha hii ya mchezaji aliyeng’ara akiwa amevaa sare namba 10.
Ortega ambaye alipewa jina la utani la The Little Donkey (Punda Mdogo), alianza kung’ara akiwa na klabu ya Atletico River Plate katika mwaka 1991 kabla ya kwenda kucheza Uturuki na Italia alikuwemo katika kikosi cha Argentina katika fainali za Kombe la Dunia za 1994, 1998 na 2002.
Unapozungumzia wachezaji nyota namba 10 wa Argentina haitakuwa haki kumuweka pembeni Pablo Cesar ambaye sasa akiwa na miaka 63 ni kocha msaidizi wa timu ya Argentina.
Mchezaji huyu kiungo alikuwa akitamba katikati ya uwanja kama yangeyange ambaye mara nyingi aliongoza mashambulizi ya kasi ya timu yake na alichezea klabu kubwa za Hispania.
Akiwa na klabu kubwa za Ureno na Hispania aliichezea Argentina mara 52, mara mbili fainali za Kombe la Dunia, mara mbili katika mashindano ya Copa America na Kombe la Mashirikisho la FIFA.
Katika orodha hii yumo kiungo Marcelo Gallardo ambaye hivi sasa akiwa na miaka 48 ni mwalimu wa klabu ya Al-Ittihad ya Saudi Arabia ambaye amechezea klabu za Argentina, nchi za Ulaya, Canada na Uruguay.
Gallardo ambaye alicheza kama kiungo alipenda mashambulizi yawe ya usawa na goli na sio pembeni.
Alichaguliwa mchezaji bora wa mwaka 2000 wa Ligi ya Ufaransa na aliichezea Argentina katika fainali mbili za Kombe la Dunia
Miongoni mwa washambuliaji wa miaka ya hivi karibuni walioipa haki yake namba 10 ni Sergio Aguero ambaye aliwika sana katika Ligi Kuu ya England na kuwa miongoni mwa wafungaji bora wa mabao akiwa na klabu ya Manchester City.
Vile vile aliichezea klabu za Atletico Madrid na Barcelona ya Hispania.
Aliteremka uwanjani na kikosi cha Argentina zaidi ya mara 100, ikiwa pamoja na katika fainali za Kombe la Dunia za 2010, 2014 na 2018.
Wachezaji wengine wanaotajwa kuwika na jezi namba 10 ni pamoja na Javier Pastore, Omar Sivori na Angel Di Maria.
Hivi sasa duniani kote mashabiki wa kandanda huvutiwa na wachezaji wanaovaa jezi namba 10, tafauti na zamani ambapo wachezaji waliopendwa zaidi walikuwa ni wale wa pembeni, namba 7 na namba 11.
Wakati ule mfumo wa mchezo ulikuwa mmoja tu, uliojulikana kama wa ‘W’ ambao ulikuwa wa mpangilio wa wachezaji kuwepo uwanjani kwa mfumo wa 1-2-1-2-5.
Katika nchi za Ulaya waliowika ni wachezaji wa pembeni kama Stanley Mathews wa England (namba7) na kule Amerika ya Kusini wachezaji kama Garincha (nambari 7).
Katika Afrika Mashariki wachezaji nambari 7 au 11 waliong’ara ni pamoja na Kalibala (Uganda), Hija Saleh (Zanzibar), Joe Kadenge (Kenya), Salim Ali Jinni na Hamisi Mtoto (Tanzania Bara).
Ilipokuja mifumo mipya ya mchezo kama 4-2-4 na 4-3-3 walichomoza wachezaji waliovaa jezi nambari 10 na kutia fora na hadi leo wachezaji wengi maarufu ni wanaovaa nambari 10 mgongoni.
Hii imesababisha mashabiki kuuliza: Kuna siri au bahati gani kwa jezi nambari 10?
Baadhi ya wachezaji siku hizi hugombea kuvaa jezi nambari 10 na inapotokea mchezaji kukubaliwa kuvaa jezi nambari 10 huwa hataki kuiachia, hata akiwa ameumia na kulazimika kukaa baoni kama mchezaji wa akiba.
Matokeo yanaonyesha wachezaji wanaovaa jezi nambari 10 siku hizi ndio wanaotegemewa sana na baadhi ya timu na wapo waliojitokeza kuwa miongoni mwa wachezaji wazuri duniani.
Wachezaji hawa wamekuwa kichocheo kikubwa cha ushindi kwa timu zao za klabu au za taifa. Hata mchezaji aliyesifika na kutajwa kuwa mfalme wa soka duniani, Edison Arantes do Nascimento (Pele) wa Brazil alivaa jezi namba 10.