USIKU wa Jumanne ulikuwa mzuri kwa timu ya taifa, Taifa Stars mara baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya timu ya taifa ya Zambia ndani ya dimba la Levy Mwanawasa katika jiji la Ndola.
Kwa ushindi huo wa bao la mapema dakika ya 5 lililofungwa na Waziri Junior Shentembo unaiweka Taifa Stars katika nafasi ya pili katika kundi E kufuzu Kombe la Dunia 2026.
Pamoja na maandalizi mazuri ya benchi la ufundi lakina jicho la kitabibu la Mwanaspoti linaona ushindi huo ulichangiwa pia na uwepo wa utimamu wa afya wa wachezaji wa kikosi hicho.
Unaweza ukawa na maandalizi mazuri lakini ukawa na wachezaji wa kikosi cha kwanza na wale ambao wako benchi wakawa hawako timamu kiafya.
Faida kubwa ambayo imeipata timu ya taifa ni kuwa ilichagua wachezaji ambao wametoka kumaliza kutumikia klabu zao katika majukumu ya ligi na mashindano mengine.
Hata wachezaji wa Yanga na Azam ambao wiki iliyopita walikutana katika fainali ngumu ya Kombe la CRDB shirikisho (FA) iliyolazimika kuchezwa dakika 120 walicheza kishujaa.
Wachezaji wa timu hizi ndio ambao walitoka katika majukumu mazito lakini walionekana kuwa timamu, hawakuonyesha hali za uchovu au kuwa na majeraha yoyote.
Hata taarifa ya msemaji wa TFF Clifford Ndimbo siku 6 zilizopita iliweka wazi kuwa wachezaji walikuwa wako timamu kiafya hawakuwa na shida yoyote ya majeraha.
Mtakumbuka kuwa timu ya taifa ilitoka kucheza na timu ya taifa ya Indonesia katika mchezo wa maandalizi wa kirafiki. Wachezaji waliocheza mchezo huo nao pia walikuwa wako imara hakukuwa shida ya kiafaya ikiwamo majeraha.
Mchezaji wa soka anakumbana na mambo mengi katika mchezo huo ambao unahusisha kutumia mwili, nguvu na kasi ili kuweza kucheza.
Hivyo ni vigumu kukosekana kwa majeraha madogo madogo mpaka makubwa ambayo yanaweza kuwapata wakati wa mazoezi na mechi.
Vijeraha vidogo vidogo vya ndani ya misuli ikiwamo michaniko ya wastani ndani ya mwili huweza kupona kwa mwili wenyewe kuweza kukarabati na kusahihisha dosari hizo.
Kadiri mchezaji anavyotumika sana katika mechi na mazoezi ndivyo pia anavyokuwa katika hatari ya kupata majeraha, hivyo ni lazima benchi la ufundi kuwa na tahadhari katika kila idara.
Idara ya Afya taifa iko vizuri, kwani inaonyesha kufuatilia ukaribu matatizo madogo madogo mpaka makubwa ya kiafya na kuchukua hatua zote za kitabibu kwa wakati.
Ukiwa na idara ya afya dhaifu katika klabu inaongeza hatari ya kuwa na wachezaji majeruhi ambao hata wakichezaji wanacheza chini ya kiwango kwani wanakuwa hawako timamu kiafya.
Mtaona pia kikosi hicho kina wachezaji vijana ikiwamo Feisal, Mudathir Yahya, Mzize, Waziri ambao umri wao ni mzuri kwa ustahimilifu dhidi ya majeraha yatokanayo na michezo.
Ingawa katika mechi hiyo dakika ya 23 Mudathir alionekana kupata shida kidogo. Lakini haijaonyesha kuwa ni shida kubwa ya kiafya.
Tatizo lingine ambalo linaweza kuchangia kuleta shida katika utimamu wa wachezaji ni uchovu wa kusafiri kutoka eneo moja kwenda lingine hasa wale wachezaji wakulipwa.
Wachezaji ambao walitoka nje ya Tanzania kama vile walifika kwa wakati na kupata mapumziko yakutosha hatimaye kuepukana na uchovu wa safari ndefu.
Vile vile timu hiyo iliondoka hapa nchini siku 6 zilizopita, walifika kule siku 3 kabla ya mechi hiyo.
Wachezaji kufika mapema katika nchi wanayokwenda kucheza ni jambo la msingi kiafya. Hii inasaidia kuweza kupata mapumziko na kuzoea mazingira ya nchi husika.
Uzuri mazingira ya Zambia hayana tofauti na ya hapa Tanzania, ipo tofouti endapo timu inayotoka uwanda wa chini kwenda kucheza katika uwanja wa juu sana au mazingira ya joto au baridi kali.
Mazingira kama hayo huitaji timu kufika mapema ili miili ya wachezaji iweze kuzoea na kunyumbulika kuendana na mazingira magumu iliyoyakuta.
Hivyo kwa Taifa Stars kufika siku 3 kabla ya mechi hiyo inasaidia wachezaji miili yao kunyumbulika kutokana na hali inayokutana nayo hatimaye kujihami mapema na mazingira yoyote.
Kama vile haitoshi upande wa hamasa na ari, hii ni kwa upande wa afya ya akili. Mchezaji lazima aandaliwe kiakili kuanzia ndani ya kikosi mpaka nje ya kikosi.
Fuko la Mama lilimwagika, hii ni baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Hassani Suluhu alitoa ahadi ya kutoa kiasi cha Sh100 milioni endapo watashinda.
Hii ni moja ya kitu kizuri kuwafanya wachezaji kuwa na hisia chanya hivyo kuwa na utulivu wakiakili hatimaye kuwa na utimamu kimwili na kiakili.
Mambo makubwa yanayolinda utimamu
Ukiacha mambo hayo hapo juu, yako mambo mengine ambayo yanatazamwa ili kulinda utimamu wa mwili.
Mchezaji anayeandaliwa kuwa mshindani ni lazima azingatie mafunzo, mazoezi ambayo yapo katika ratiba ya wakufunzi. Benchi dhaifu la ufundi huwapa mazoezi yasiyo na kipimo.
Uwepo wa benchi bora la ufundi huwapa mazoezi yanayoendana na muongozo wa sayansi ya michezo hatimaye kuweza kutowapa wachezaji majeraha.
Lishe, wachezaji wanapopata lishe ambayo imeshauriwa na wataalam wa afya ikiwamo wale wa lishe ina maana kuwa wanapata lishe sahihi hatimaye kuwa na afya bora.
Kupumzika, kulala na burudisho tulizo. Mchezaji anapofanya mazoezi na kula lishe huitaji mambo haya matatu ili kuufanya mwili kuwa na kinga imara hatimaye utimamu bora wa mwili.
Usimamizi wa nidhamu, uongozi bora wa timu unachangia wachezaji kuwa na nidhamu ya hali ya juu.
Hii inawafanya wachezaji kutokuwa na mienendo mibaya ya kimaisha ikiwamo ulevi, utumiaji tumbaku, uvivu, maisha ya anasa na ulaji holela.