‘Msibebe wagombea mifukoni, tendeni haki’

Iringa. Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Daudi Yassin amesema ikiwa viongozi wataleta mizengwe kwenye chaguzi za ndani za CCM kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa ni rahisi kushindwa.

Amesema badala ya kubeba wagombea mifukoni wanatakiwa kuhakikisha kuwa wanatenda haki kwa kuwachagua wanachama wanaokubalika.

Yassin amesema hayo katika ziara yake ya siku moja aliyoifanya leo Juni 12, 2024 kwenye kata za Nyalumbu na Ilula wilayani Kilolo.

“Mkileta mizengwe tutapigwa Serikali za mitaa, uchaguzi wa mitaa na vijiji ni rahisi sana tendeni haki, angalieni watu wanamtaka nani,” amesema Yassin na kuongeza;

“Usitumie nafasi yako vibaya kumpiga zengwe mtu kwa sababu una chuki naye, tumia dhamana yako ya uongozi kutenda haki, weka mbele masilahi ya CCM sio yako.”

Aidha, amewataka viongozi wa vijiji kusoma mapato na matumizi na kuwa wawazi katika kuwatumikia wananchi.

“Isipokuwa muwazi, usiposoma mapato na matumizi kijijini kila baada ya miezi mitatu itakugharimu mwenyewe siku ya kupigiwa kura ikifika,” amesisitiza.

Amewashauri viongozi hao kutimiza wajibu wao kwa kufanya kazi kwa bidii, kusikiliza kero za wananchi  na kuzitatua.

“Serikali hii inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ni ya wananchi. Kazi yetu viongozi ni kuhakikisha tunasikiliza changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi,” amesema Yassin.

Amesema kitakachosababisha CCM iendelee kubaki madarakani ni uwajibikaji wa viongozi kila mmoja kwenye eneo lake.

“Hakuna muujiza, tumeagizwa kufanya kazi tukafanye kazi, tuwajibike kila mtu. Changamoto zilizopo ni kujitafutia majibu,” amesema Yassin.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kilolo, John Kiteve amesema wamejiandaa vyema kuhakikisha kuwa wanashinda uchaguzi wa Serikali za mitaa.

Kwa upande wa Katibu wa Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM) Mkoa wa Iringa, Aisha Mpuya amesema ziara hiyo pamoja na mambo mengine inalenga kuimarisha chama hicho kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka huu.

Related Posts