Mzambia alia na kina Bacca

KOCHA wa Zesco United ya Zambia,  George Lwandamina ameshangaa kuona mabeki wawili wa Taifa Stars na Yanga nahodha Bakari Mwamnyeto na Ibrahim Hamad ‘Bacca’, wakiendelea kucheza soka la ndani kutokana na ubora walionao, huku akifichua kilichomfanya aondoke uwanjani wakati wa mechi ya Zambia na Tanzania.

Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Ndola, Zambia mara baada ya Stars kuichapa Zambia kwa bao 1-0, katika mchezo wa kuwania fainali za Kombe la Dunia 2026, Lwandamina alisema mabeki licha ya Stars kucheza kwa malengo lakini wao ndio walimaliza Chipolopolo.

Lwandamina alisema washambuliaji wa Zambia wakiongozwa na Patson Daka, walishindwa kukamilisha mashambulizi kutokana na uimara wa wa mabeki hao kwa kuwazima kwa mashambulizi ya juu na chini.

Kocha huyo wa zamani wa Yanga na Azam alisema kipa wa Stars, Ally Salim, alikuwa na mchezo mzuri kutokana na uimara wa mabeki hao waliofanya kazi kubwa kupunguza makali ya Wazambia.

“Ilipofika dakika ya 89 nilichukua uamuzi wa kuondoka uwanjani, sikuona nafasi ya Zambia kupata bao tena kwani washambuliaji wetu walikuwa wanaongeza presha wakati mabeki wa Tanzania wakiendeleza ubora wao,” alisema Lwandamina na kuongeza;

“Wale mabeki wawili wa kati Bakari (Mwamnyeto) na Ibrahim (Hamad) walicheza vizuri, kawaida yale mashambulizi ya Daka katika mechi zingine asingetoka bila bao lakini alibanwa sana aliporuka na hata alipotaka kushambulia kwa miguu.

“Siku zote huwa nashangaa kwanini Tanzania mabeki kama hawa bado wako ndani nadhani kuna nafasi mawakala hawawatendei haki, kwani ni mabeki wanakaba kisasa sana, niliwaona tangu katika fainali za Afcon 2023, kule Ivory Coast.”

Staa wa KMC na Taifa, Waziri Junior, amefunguka mambo makubwa matatu aliyoyapata baada kufunga bao pekee katika mechi hiyo hatua ya makundi.

Alieleza, anajihisi furaha sana kwa ushindi, lakini yapo mambo yaliyoongezeka kwake baada ya kucheza kwa mara ya kwanza na kufunga.

“Kupangwa kucheza kwangu ilikuwa kama taarifa ya ghafla sikutarajia lakini nilipoingia akili yangu ilikuwa iko tayari kuipambania timu na taifa kwa ujumla,

Nimetoka uwanjani nikiwa nimeongezeka vitu vitatu kujiamini, naweza kufanya chochote wakati wowote,utulivu wa akili kwani bao nililofunga bila utulivu nisingefunga na ujuzi umeongezeka, nimecheza na wachezaji tofauti wenye uwezo mkubwa,” alisema Waziri aliyewataja makocha wa timu hiyo na kipa Aboutwalib Mshery kumjaza upepo mapema.

“Kabla ya mechi kipa Abdutwalib Mshery alinipa maneno ya kijasiri na kuniambia hakuna kigeni kwenye mpira kwahiyo nenda kapambaneni, makocha walifurahi na kuniambia niendelee kupambana kwani sio mwisho,” alisema Waziri Jr na kuongeza;

“Ameona utofauti mkubwa ndani ya timu ya Taifa kwani wachezaji wamekuwa na ushirikiano bila kujali tumetokea wapi na morali ya kuipambania timu kwa umoja.”

Stars sasa ipo nafasi ya pili katika Kundi E hilo inayoongozwa na Morocco.

Related Posts