Dar es Salaam. Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limesema kiasi cha Sh2.6 bilioni zitaokolewa kwa mwezi ambazo ni zaidi ya Sh30 bilioni kwa mwaka zinazotumiwa kununua umeme nchini Uganda unaotumika mkoani Kagera.
Hatua ya kuokoa fedha hizo imekuja kufuatia Tanesco kusaini mkataba na Mhandisi mshauri kutoka nchini Misri (Shaker Consultancy Group) atakayesimamia ujenzi wa mradi wa umeme mkoani Kagera.
Mradi huo utahusisha ujenzi wa njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 220 kutoka Benaco hadi Kyaka mkoani Kagera ambapo ukikamilika utawezesha wilaya za mkoani humo kuingizwa kwenye gridi ya Taifa na kuacha kutumia umeme kutoka Uganda.
Akizungumza leo Juni 12, 2024 jijini hapa wakati wa utiaji saini mkataba huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga amesema kampuni ya Shaker ndio itakayotafuta mkandarasi atakayejenga mradi huo na kuusimamia.
“Mradi huu utaanza ujenzi Januari mwaka 2025 ila kwa sasa Kampuni ya Shaker itatafuta mkandarasi. Mradi utatumia miezi 24 hadi kukamilika kwake hivyo ifikapo Desemba 2026 utakamilika na wilaya za mkoa huo zitaingizwa kwenye gridi ya Taifa,” amebainisha.
Akifafanua zaidi Nyamo-Hanga amesema kwa sasa Kagera inatumia megawati 21 kwa mwezi inazonunua kutoka Uganda, hivyo faida ya mradi huo ni kuokoa zaidi ya Sh2.6 kwa mwezi.
“Wilaya za Kyerwa, Karagwe, Misenyi, Muleba, Bukoba vijijini na Manispaa ya Bukoba kwa muda mrefu zimekuwa zikitumia umeme kutoka Uganda.”
“Ujenzi wa mradi huu utagharimu Dola za Marekani milioni 135.4 ukihusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya umbali wa kilomita 166.17 kutoka Benaco mpaka Kyaka, ujenzi wa kituo kipya cha kupoza umeme cha Benaco na kukiongezea uwezo kituo cha kupoza umeme Kyaka kilichopo sasa,” amebainisha.
Amesema mradi huo utahusisha kandarasi tatu ambazo ni ujenzi wa kituo cha kupooza umeme wa kilovoti 220 kushusha hadi kilovoti 30, pili ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa kilovoti 220 yenye urefu wa kilomita 166.17 kutoka Benaco hadi Kyaka na tatu ni ujenzi wa miundombinu ya kusafirisha umeme wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilomita 683 na mashine ndogo katika vijiji umeme huo utakapopita.
Fedha hizo za ujenzi zitagharamiwa na Serikali ya Tanzania kiasi cha Sh6.2 bilioni, Mfuko wa Maendeleo wa Saudi (SFD) Dola za Marekani milioni 13, Mfuko wa Maendeleo wa Abu dhabi Dola za Marekani milioni 30 na Mfuko wa Maendeleo ya Kimataifa wa OPEC ambao utachangia kiasi cha Dola milioni 60 za Marekani.
Aidha, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Shaker Consultancy Group, Dk Ismail Shaker amesema wana uzoefu wa kufanya kazi nchini kwa muda mrefu, huku akiahidi kukamilisha mradi huo kwa wakati.