Yanga kwanza, Simba yamgeukia Dube

SIMBA imemuwekea Prince Dube Sh.120Mil mezani ili amwage wino wakamalizane na Azam, akawachomolea waziwazi.

Mwanaspoti limeambiwa kuwa Dube amewaambia tayari ana makubaliano na klabu moja ya Tanzania ambayo anaipa kipaumbele kikubwa na hata wasimamizi wake wamekomalia kwenye hilo.

Yanga inatajwa kuwa nyuma ya sakata la Dube kwani mara kadhaa ameonekana akiwa na watu wa karibu ya uongozi wa juu wa klabu hiyo na ingawa ana kesi ya msingi na Azam ambayo haijatolewa uamuzi kwenye mamlaka za soka za Tanzania.

Simba imedaiwa kumshawishi Dube ikijaribu bahati kama atakubaliana na ofa hiyo waliyompelekea mezani kisha wakimtaka mambo ya klabu aliyokuwa akiichezea Azam wawachie wao watajua jinsi ya kumalimaliza na matajiri hao wa Chamazi.

Ikumbukwe Simba awali ilishapewa ruksa na Azam kuzungumza na Dube lakini badae klabu hiyo ikaja kudai kwamba mzigo Mnyama alioweka mezani ulikuwa haukidhi Sh700Mil wanazotaka.

Habari za ndani zinasema Simba imeweka ofa ya Sh 120 Milioni kwa Dube kama atakubali mkataba wa miaka miwili, lakini ajabu ni kwamba Mzimbabwe huyo amewasisitiza  “hapana wasubiri kwanza.”

“Unajua Dube anajua wapi anataka kwenda na huyu sio mchezaji anayeongozwa na tamaa, anasubiri maamuzi ya kamati kisha atajua wapi atakwenda baada ya hili suala kumalizika,” kilisema chanzo hicho kilichokaribu na Dude na kufichua kwamba wapambe wanaojitanabaisha na Yanga wamempangia nyumba ya kifahari maeneo ya Salasala Dar es Salaam na kumpa ulinzi na gari ya kifahari.

Huku upande wa Dube ukiwatuliza Simba Mwanaspoti linafahamu kwamba mshambuliaji huyo alishapewa mkataba wa awali wa miaka miwili na Yanga kisha kila upande kukubaliana kukausha kimya kama vile hawajuani.

Dube alichagua kuitumikia Yanga ambapo hatua ya Simba kumfuata ingekuwa ngumu kuvamia ofa yao kwa vile tayari ameshamalizana kila kitu na mabingwa hao wanaotajwa kumgharamia kila kitu na ameanza kuzoeana taratibu na mastaa wa Jangwani ambapo Aziz Ki alijisahau wiki hii na kutamka wazi kwamba ; “kazi ya kufunga msimu ujao ni ya Dube, Dube anakuja.”

Licha ya Dube kuondoka Azam, klabu hiyo imeonyesha kumfungia vioo baada ya kuondoa picha yake katika bango ya kikosi cha timu hiyo kilichosherehekea kushika nafasi ya pili katika ligi na kukata tiketi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.

Dube aliyesaliwa na Azam mwaka 2021  anasikilizia hukumu ya kesi yake na Azam.

Related Posts