Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ametaka aina mbalimbali za sanaa zitumike katika usambazaji wa matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022.
Msingi wa kauli yake hiyo ni kile alichoeleza, sanaa ndiyo itakayofanikisha ufikishaji wa taarifa za sensa ya watu na makazi kwa wananchi wengi.
Katika hoja yake hiyo, amewataka wasanii kuhakikisha wanafanikisha hilo, kama ambavyo wamekuwa wakitumika kufikisha taarifa mbalimbali kwa wananchi kutokana na umaarufu wao.
Chalamila ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam leo Jumatano Juni 12, 2024 alipozungumza na wasanii katika ukumbi wa Kiramu uliopo Mbezi Beach.
Amewataka wasanii wa aina zote kuhusika kikamilifu katika usambazaji wa matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 kwenye sanaa zao.
“Nyinyi ni miongoni mwa watu wachache ambao mmebarikiwa kuwa na vipaji maalumu ambavyo vimekuwa na tija na mchango katika Taifa letu,” amesema.
Amefafanua kuwa kutokana na mchango wao mkubwa wa kufikisha taarifa kwa umma, ndiyo maana viongozi mbalimbali wanawatumia hasa kipindi cha uchaguzi ili mambo yao yawafikie watu wengi. “Pia jiandaeni mambo mazuri yanakuja.”
Akizungumza kwenye mkutano huo wa wasanii Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule amewataka kushirikiana kwenye kupinga ubaki, ulawiti, ukatili wa kijinsia maswala ya lishe na usafi.
“Twendeni tukaihabarishe jamii kuhusu masuala haya na kupitia kwenu hili linawezekana.”
Naye Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa Tanzania (Basata), Dk Kedmon Mapana amesema, “leo tupo hapa kwa ajili ya kupokea takwimu hizi, sio kupokea tu lakini namna gani tunakwenda kuzitumia na kuelimisha jamii kuhusiana nazo ndilo jambo muhimu, hivyo kama ilivyosemwa awali nendeni mkaijuze jamii kuhusu takwimu hizi.”